1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Mali yazuia jaribio la mapinduzi

17 Mei 2022

Serikali ya Mali inayoongozwa na rais aliyefanya mapinguzi mara mbili imetangaza kuwa vikosi vyake vya usalama vimezuia jaribio la mapinduzi ambalo imesema liliungwa mkono na nchi moja ya Magharibi ambayo haikutajwa.

https://p.dw.com/p/4BO8F
Mali | Colonel Assimi Goita
Picha: Annie Risemberg/AFP

Tangazo hilo ni msukosuko wa hivi punde zaidi kutokea Mali, ambako Kanali Assimi Goita aliongoza mapinduzi mara mbili katika mwaka wa 2020 na 2021 kabla ya kuwa rais wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

Soma pia: Chanzo cha mzozo wa Mali na mshirika wake Ufaransa

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga haikuitaja nchi ambayo inatuhumiwa kuunga mkono njama ya mapinduzi. Hata hivyo, mahusiano na mtawala wake wa zamani Ufaransa yamedorora pakubwa chini ya uongozi wa Goita, hali iliyolilazimu jeshi la Ufaransa kuanza kuwaondoa askari wake ambao walikuwa nchini humo kwa miaka tisa wakipigana na wanamgambo wa itikadi kali.

G5 Sahel
Mali imetangaza kujiondoa katika jeshi la kikanda la G5Picha: Bourema Hama/AFP/Getty Images

Akizungumza kwenye televisheni, Maiga amesema bila kutoa maelezo zaidi kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilizimwa Jumatano wiki iliyopita. "Serikali ya Jamhuri ya Mali inalaani, vikali kabisa, kitendo hiki cha kuchukiza sana kwa usalama wa taifa letu, ambapo lengo lilikuwa ni kuzuia au hata kuangamiza juhudi kubwa za kuilinda nchi yetu na kurejea kwa utaratibu wa kikatiba unaohahakikisha amani na utulivu."

Amesema usalama umeimarishwa kwenye vituo vya ukaguzi kwenye barabara za kuondoka mji mkuu Bamako ili kuwasaka wahusika.

Tuhuma hizo za kuingiliwa na nchi za kigeni zinakuja wakati utawala wa Goita ukiendelea kutengwa. Siku moja kabla, msemaji huyo wa serikali alikuwa ametangaza kuwa Mali inajiondoa kwenye jeshi la usalama wa kikanda la mataifa matano linalofahamika kama G5.

Na mwezi uliopita ilisema inavifungia milele vyombo vya habari vya Ufaransa, Radio France International na France 24, ambavyo ni vyombo viwili vyenye wasikilizaji wengi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Ufaransa na mataifa mengine yalilaani mapinduzi ya Agosti 2020 ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia Ibrahim Boubacar Keita. Miezi tisa baadaye, Goita akafanya mapinduzi kwa mara ya pili wakati alipowatimua viongozi wa kiraia wa mpito na mwenyewe akachukua madaraka kama rais.

Wakati utawala wa kijeshi awali ulikubali kipindi cha mpito cha miezi 18 kurejesha madaraka ya kwa utawala wa kiraia, ulishindwa kuandaa uchaguzi kabla ya muda wa mwisho wa Februari. Mwezi uliopita, serikali ilisema inahitaji miaka mingine miwili madarakani kabla ya kuandaa uchaguzi.

AP