Watu 50 wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
3 Januari 2025Mashambulizi hayo ya anga ya Israel yaliyoanza jana na kuendelea siku ya Ijumaa, yaliyalenga maeneo ya kati ya Deir al Balah na kusini mwa Gaza huko Khan Younis ambapo maafisa watano wa polisi wameuawa.
Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer amesema shambulio hilo lilikuwa likimlenga afisa mwandamizi wa Hamas huku ikilitupia lawama kundi hilo kwa vifo vya raia.
"Shambulio la anga lililoongozwa na idara ya ujasusi usiku kucha, lilimlenga Hossam Shahwan, mkuu wa kikosi cha usalama wa ndani cha Hamas kusini mwa Gaza. Tumempata wapi? Si mahali pengine, bali alikuwa kajificha katika eneo la kiraia huko Khan Younis, ambapo raia wa Gaza wamejihifadhi ili kujikinga na vita hivi, " alisema Mencer.
Kambi ya al-Mawasi inayowahifadhi Wapalestina kwenye mahema ambayo mara kadhaa Israel imeitaja kuwa eneo salama la kibinadamu imeshambuliwa pia.
Juhudi za kusitisha mapigano Gaza zaendelea
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema imeidhinisha ujumbe kutoka idara ya upelelezi (Mossad) na ile ya usalama wa taifa (Shinbet) ili kuendelea na mazungumzo nchini Qatar kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza. Ujumbe huo unatarajiwa kusafiri leo Ijumaa. Kwa sasa Hamas haijazungumza chochote kuhusu hilo.
Wapatanishi kutoka Marekani, Qatar na Misri wametumia karibu mwaka mmoja kujaribu kufikiwa kwa mpango wa usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka, lakini mara kadhaa juhudi zao zimekuwa zikiambulia patupu.
Vita vya Israel huko Gaza vilivyoanza Oktoba 7 mwaka 2023 baada ya Hamas kuvamia kusini mwa Israel na kuua watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200, vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 45,500, hii ikiwa ni kulingana na maafisa wa afya wa eneo hilo, ambao wanasema wanawake na watoto wanachangia zaidi ya nusu ya idadi hiyo ya vifo.
Soma pia: Amnesty International yaishtumu Israel kwa mauaji ya halaiki katika ukanda wa Gaza
Mamlaka ya afya inayodhibitiwa na Hamas haitofautishi vifo vya raia na wapiganaji ambapo jeshi la Israel linadai tayari limewaua wapiganaji 17,000 wa Hamas bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote.
Hayo yakiarifiwa, jeshi la Israel limesema lilidungua kombora lililorushwa kutoka Yemen baada ya kuvuka mpaka na kuingia katika ardhi ya Israel mapema leo Ijumaa katika eneo la katikati mwa nchi hiyo la Modi'in.
Waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran na wanaodhibiti sehemu kubwa ya Yemen, wamekuwa wakirusha makombora na droni kuelekea Israel, pamoja na kushambulia meli katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, kwa kile wanachosema ni kudhihirisha mshikamano na Wapalestina katika vita vya Israel na Hamas huko Gaza.
(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)