Watu 41 wauawa katika shambulizi la shule Uganda
17 Juni 2023Maafisa nchini Uganda wamepata miili 42 ya watu, wakiwemo wanafunzi 38, waliochomwa moto, kupigwa risasi au kukatwakatwa hadi kufa baada ya waasi kuishambulia shule ya sekondari karibu na mpaka na Kongo. Jeshi la Uganda limesema karibu watu sita walitekwa nyara na waasi hao, ambao walivuka mpaka na kuingia upande wa Kongo baada ya uvamizi huo wa Ijumaa usiku.
Maafisa wamesema mauaji hayo katika shule ya sekondari ya Lhubiriha katika mji wa mpakani wa Mpondwe yalifanywa na waasi wa itikadi kali wa ADF, ambao wamekuwa wakishambulia kwa miaka mingi kutokea mashariki mwa Kongo. Meya wa Mpondwe, Selevest Mapoze amesema wahanga ni pamoja na wanafunzi, mlinzi mmoja na wanakijiji wawili.
Msemaji wa jeshi Brigedia Felix Kulayigye amesema shambulizi hilo liliwahusisha washambuliaji watano. Amesema askari kutoka kambi iliyo karibu walifika katika eneo hilo na kukuta shule ikiwa inawaka moto, huku miili ikiwa imetapakaa. Vikosi vya usalama vinaendelea na msako dhidi ya wavamizi hao waliokimbilia Mbuga ya Kitaifa ya Virunga.
Soma pia: Wakuu wa majeshi wa Uganda na Kongo wakutana Beni
Msemaji wa polisi Fred Enanga amesema ADF ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waliishambulia shule ya sekondari ya Lhubiriha katika eneo la Mpondwe Ijumaa usiku ambapo bweni lilichomwa moto na ghala la chakula kuporwa.
Shule hiyo iko umbali wa karibu kilomita mbili kutoka mpakani. Mkuu wa Wilaya Joe Walusimbi aliliambia shirika la Habari la AFP kuwa wanafunzi kadhaa hawajulikani waliko. Enanga amesema jeshi na polisi wanawasaka washambuliiaji hao waliokimbilia upande wa Mbuga ya Kitaifa ya Virunga kuingia upande wa Kongo.
Soma pia; Zaidi ya watu 70 wauwawa na ADF Kongo
Msitu huo mkubwa ulioko kwenye mpaka wa Uganda na Rwanda, hutumiwa kama maficho na wanamgambo ambao wanaendesha harakati zao mashariki ya Kongo.
Waasi wa ADF walianzia harakati zao nchini Uganda, kabla ya kurufushwa na kukimbilia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika miaka ya 1900 na tangu hapo wanatuhumiwa kwa kuwauwa maelfu ya raia.
Tangu mwaka wa 2019, baadhi ya mashambulizi ya ADF mashariki mwa Kongo yamedaiwa kufanywa na kundi la IS, ambalo linawaelezea wapiganaji hao kuwa tawi lao, la IS katika kanda ya Afrika ya Kati.
Sio shambulizi la kwanza kwenye shule nchini Uganda linalohusishwa na waasi hao. Mnamo Juni 1998, wanafunzi 80 waliteketea kwenye moto katika mabweni yao kufuatia shambulizi la ADF kwenye Taasisi ya Ufundi ya Kichwamba karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Zaidi ya wanafunzi 100 walitekwa nyara.
Uganda na Kongo zilianzisha operesheni ya pamoja mwaka wa 2021 kuwafurusha waasi wa ADF kutoka ngome zao za nchini Kongo, lakini hatua hizo zimeshindwa kukomesha mashambulizi ya kundi hilo. Mnamo Machi mwaka huu, Marekani ilitangaza zawadi ya hadi dola milioni 5 kwa yeyote atakayetoa Habari ya kukamaztwa kiongozi wa ADF Musa Baluku.
Afp, ap