1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNigeria

Watu 21 wauawa katika shambulizi la genge nchini Nigeria

Saleh Mwanamilongo
11 Januari 2025

Msemaji wa polisi ya Nigeria, Abubakar Sadiq Aliyu, amesema msafara wa wanamgambo wa serikali ulishambuliwa kwa bunduki na majambazi huko Baure, kijiji katika wilaya ya Safana.

https://p.dw.com/p/4p3iW
Polisi imesema shambulizi hilo lilifanyika Ijumaa katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina nchini Nigeria
Polisi imesema shambulizi hilo lilifanyika Ijumaa katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina nchini NigeriaPicha: Afolabi Sotunde/REUTERS

Wanamgambo wapatao 21 wanaoiunga mkono serikali ya Nigeria wameuawa katika shambulizi la kuvizia na magenge ya wahalifu. Polisi imesema shambulizi hilo lilifanyika Ijumaa katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina nchini Nigeria.

Msemaji wa polisi ya Nigeria, Abubakar Sadiq Aliyu, amesema msafara wa wanamgambo wa serikali ulishambuliwa kwa bunduki na majambazi huko Baure, kijiji katika wilaya ya Safana. Aliyu aliongeza kuwa polisi walikuwa wakiwatafuta wahusika.

Jimbo la Katsina ni mojawapo ya majimbo kadhaa kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria yanayotishiwa na majambazi wanaovamia vijiji, kuwaua na kuwateka nyara wakaazi pamoja na kuzichoma moto na kuzipora nyumba.

Magenge hayo, ambayo yana kambi zao katika msitu mkubwa unaoyazunguka majimbo ya Zamfara, Katsina, Kaduna na Niger, yanatajwa kuhusika na utekaji nyara mkubwa wa wanafunzi wa shule katika miaka ya hivi karibuni.