Watu 2 wauwawa katika maandamano ya Narok
27 Januari 2015Viongozi wa kaunti ya Narok nchini Kenya wameitwa makao makuu ya idara ya upelelezi kujibu maswali mbalimbali kuhusiana na machafuko yaliyozuka katika maandamano ya jana katika eneo la mbuga ya wanyama ya Maasai Mara mjini Narok juu ya makusanyo ya fedha za utalii na fursa za ajira kwa wazawa kwenye vivutio vya watalii, ambapo watu wawili waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mkurugenzi wa idara ya upelelezi Ndegwa Muhoro amesema viongozi wameitwa aktika ofisi yake jijini Nairobi kujibu maswali katika uchunguzi unaofanywa kubaini nani mwenye dhamana kwa maandamano hayo yaligubikwa namachafuko. Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi huku waandamanaji wakiwarushia mawe.
Maelfu ya watu wakiongozwa na mbunge wa eneo hilo waliandamana katika ofisi za serikali ya kaunti ya Narok, kiasi kilometa 140 magharibi mwa mji mkuu, Nairobi. Magazeti ya Kenya yameripoti watu wawili walipigwa risasi na kuuwawa na wengine sita kujeruhiwa, lakini maafisa wanasema mtu mmoja tu alikufa. Waandamanaji wanadai gavana wa Narok, Samuel Ole Tunai, hakuweza kutoa malezo kuhusu matumizi ya mabilioni ya shilingi za Kenya, zikiwemo fedha za mapato kutokana na utalii na fedha kutoka serikali kuu.
Je wanaharakati wa kutetea haki za raia nchini Kenya wanasemaje kuhusu yaliyojiri katika maandamano hayo? Josephat Charo amezungumza na Okiya Omatatah Okoiti, ambaye ni mwanaharakti wa haki za raia mjini Nairobi.
Mwandishi: Josephat Charo/afp
Mhariri: Mohammed Khelef