Watu 16 wameuawa mashariki mwa Ukraine
6 Septemba 2023Rais Volodymyr Zelensky ameonya kuwa idadi ya majeruhi inaweza kupanda zaidi. Hayo yanajiri wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken akifanya ziara ya ghafla mjini Kyiv.
Soma pia:Urusi yafanya mashambulio ya Droni katika mji Odessa
Rais Volodymyr Zelenskiy amelaani shambulio hilo, lililolenga soko na duka la dawa katika mji wa viwanda wa Kostyantynivka, kilomita 30 kutoka mji wa Bakhmut, ambao umeshuhudia mapigano makali kwa miezi kadhaa.
Maafisa wa Ukraine wamechapisha video kwenye mtandao wa Telegram ambayo inaonyesha mlipuko mkubwa , huku watu wakianguka chini na wengine wakikimbia na kujificha. Vyombo vya habari vya ndani vimeelezea kuwa ni shambulio la kombora.
Rais Volodymyr Zelensky amesema uovu huo wa Urusi lazima ushindwe haraka iwezekanavyo.
Soma pia: Urusi yasema imezima jaribio dhidi ya daraja la Crimea
Waziri wa Ukraine wa Mambo ya Ndani Ihor Klimenko amesema waliouwawa ni pamoja na raia 16 na takriban wengine 28 wamejeruhiwa. Picha zilizowekwa kwenye mtandao wa Telegram zinazoonyesha waokoaji wakiendelea na juhudi za kuwaokoa watu waliokwama kwenye vifusi.
Ziara ya Blinken Kyiv
Ni katika mazingira hayo ndio waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken aliwasili mjini Kyiv hii leo. Blinken amesema ziara hiyo ni ishara ya kuiunga mkono Ukraine dhidi ya vikosi vya Urusi.
"Tumeona maendeleo mazuri katika mashambulizi ya kujibu. Inatia moyo sana. Tunataka kuhakikisha kwamba Ukraine ina kila inachohitaji, sio tu kufanikiwa katika mapambano dhidi ya mashambulizi, lakini ina kila inachohitaji kwa muda mrefu ili kuhakikisha kuwa ina kizuizi chenye nguvu, uwezo thabiti wa ulinzi, ili katika siku zijazo uchokozi kama huu usitokee tena.'' amesema Blinken.
Wakati huohuo ujumbe wa juu wa bunge la Marekani unakutana na mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC Karim Khan, mjini The Hague, kujadili tuhuma za uhalifu wa kivita dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin. Ujumbe huo umeongozwa na Michael McCaul, Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya baraza la wawakilishi kutoka chama cha Republican.
Soma pia: Marekani kujadiliana na ICC juu ya uhalifu dhidi ya Putin
Rais wa Romania Klaus Iohannis amesema hii leo kuwa ikiwa sehemu ya droni ilioanguka wiki hii katika ardhi yake itathibitishwa kuwa ni ya Urusi basi itakuwa ukiukaji mkubwa wa uhuru wa nchi yake.
Kwa upande wake waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema nchi yake imepanga kuongeza kwa kiasi kikubwa ununuzi wa silaha katika mwaka ujao wa 2024. Amesema Ujerumani ni wafadhili wa pili kwa ukubwa kwa Ukraine baada ya Marekani.