1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 10 wamekufa Marekani baada ya dereva kuparamia umati

1 Januari 2025

Watu wasipungua 10 wamekufa na zaidi ya wengine 35 wamejeruhiwa baada ya dereva kulivurumisha lori lake kwenye umati wa watu waliokuwa wanasherekea Mwaka Mpya huko New Orleans, Marekani.

https://p.dw.com/p/4ojjV
Eneo la mkasa huko New Orleans, Marekani
Eneo la mkasa huko New Orleans, Marekani.Picha: MATTHEW HINTON/AFP

Hayo yameelezwa na Shirika la Upelelezi la Marekani ambalo limearifu kwamba linachunguza kisa hicho kama tukio la kigaidi.

Tukio hilo limetokea mnamo saa tisa alfajiri kwa saa za Marekani kwenye makutano ya mitaa ya Canal na Bourbon wakati watu wakiwa wanafanya shereha za kuanza kwa mwaka mpya 2025.

Mtaa wa Bourbon ni eneo maarufu la watalii kwenye mji mdogo wa French Quarter, na linafahamika kwa kuvutia makundi makubwa ya watu wanaotembelea kumbi za starehe na vilabu vya pombe.

Mkuu wa polisi Anne Kirkpatrick amesema "Mwanaume huyo alijaribu kuwadhuru watu wengi zaidi kadri alivyoweza."

"Alikuwa amedhamiria kusababisha balaa kubwa na uharibifu wa kutisha ambao ameufanya" amesema afisa huyo wa ngazi ya juu wa polisi.

Kirkpatrick amesema dereva huyo pia aliwashambulia kwa risasi polisi na kuwajeruhi askari wawili baada ya lori lake kupinduka. Dereva huyo aliuawa eneo la tukio baada ya makabiliano na maafisa wa usalama.

"Tunafahamu mshambuliaji ameuawa," amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa New Orleans, Oliver Thomas. Hadi sasa utambulisho wa dereva huyo bado haujatolewa.

FBI yasema inachunguza mkasa huo kuwa ugaidi na Biden atuma salamu za pole

Afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la FBI kwenye ofisi wa New Orleans, Alethea Duncan, hapo mwanzo alisema mkasa huo siyo tukio la kigaidi lakini baadaye FBI ilisema itachunguza mkasa huo kwa mwelekeo wa kuwa shambulio la kigaidi.

Marekani | New Orleans, eneo la mkasa
Polisi wakishika doria kwenye mkasa wa kuvurumishwa gari kwenye umati wa watu huko New Orleans, Marekani.Picha: MATTHEW HINTON/AFP

Moja ya shuhuda wa mkasa huo Kevin Garcia, 22, amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kwamba aliona lori likiwaparamia watu kando kwenye njia ya wenda kwa miguu na akasikia milio ya risasi.

"Mwili wa mtu mmoja ulipita mbele ya macho yangu," amesema kijana huyo na kuongeza kwamba alisikia vilio na mayowe huku watu wakitimua mbio.

Wale waliojeruhiwa kwenye mkasa huo wamepelekwa kwenye hospitali tano za mji. Hayo yamefahamishwa na idara ya dharura ya mji huo.

Ikulu ya Marekani imesema Rais Joe Biden alifahamishwa mara moja juu ya tukio hilo na amefanya mazungumzo na meya wa mji huo kuonesha uungaji mkono wa serikali kuu mjini Washington.