Watu 10 wakiwemo watoto 2 wauawa kwa bunduki Montenegro
2 Januari 2025Watu 10 wakiwemo watoto wawili wameuawa nchini Montenegro katika shambulizi la bunduki lililotokea kwenye mji wa kusini wa Cetinje. Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Danilo Saranovic, amesema mshambuliaji aliyejihami kwa bunduki na kutambuliwa na polisi kama Aleksandar Martinovic, amefariki kutokana na majeraha baada ya kujaribu kujiua wakati akikimbizwa hospitali.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Milojko Spajic ameongeza kuwa watu wengine wanne wamejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo na wanapatiwa matibabu hospitalini katika mji mkuu wa Podgorica.
Soma: Montenegro yapiga kura katika uchaguzi wa bunge
Hapo awali, polisi walikuwa wamesema kuwa mauaji hayo yalitokea katika mgahawa mmoja lakini baadae mkuu wa polisi aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mauaji hayo yalitokea katika maeneo manne tofauti. Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo.