Wataalamu wa Umoja wa Mataifa: Rwanda inashirikiana na M23
5 Agosti 2022Katika ripoti mpya kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, wataalamu hao wamevilaumu vikosi vya Rwanda kwa kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu silaha dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kutokana na uingiliaji wake wa moja kwa moja katika taifa hilo tangu Novemba mwaka jana hadi Juni mwaka 2022, ama kwa kuliunga mkono kundi la waasi la M23 au kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya kundi jengine la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda, FDLR.
Kundi hilo la wataalamu limeongeza kuwa wanajeshi wa Rwanda walikiuka pia vikwazo kwa kutoa silaha, risasi na sare za kijeshi kwa waasi hao wa M23.
Ripoti hiyo imesema licha ya takriban miezi 15 ya hali ya dharura inayoendelea kuiweka chini ya mamlaka ya kijeshi mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo pamoja na operesheni za kijeshi zinazofanywa na majeshi ya nchi hiyo, vikosi vya Uganda, na wanajeshi kutoka kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO, hali ya usalama na kibinadamu katika maeneo hayo mawili imebaki kuwa ya kutia wasiwasi mkubwa.
Soma zaidi: Congo kutathmini upya muda wa MONUSCO kuondoka DRC
Wataalamu hao pia walitaja hali inayozidi kuzorota katika maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo Kaskazini mwa Kivu, huku wakibaini kuwa mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa M23 yamekuwa ya mara kwa mara, marefu na thabiti na kwamba eneo wanalolidhibiti limeongezeka mno na kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao huku pia kukiwa na mashambulizi ya kiholela.
Ripoti hiyo imesema kuwa waasi hao wa M23 wanawauwa raia kwa makusudi na kutumia mbinu ya kuvishambulia vikosi vya MONUSCO.
Vikosi vya Kongo vyadaiwa kujiunga na makundi yanayojihami
Wataalamu hao wanasema baadhi ya vikosi vya Jamhuri ya kideomkrasi ya Congo viliingia katika ushirikiano wa muda na makundi ya kujihami katika eneo hilo ili kupambana na waasi wa M23 na kuwa makundi hayo ya kujihami yalipewa silaha, risasi na sare na baadhi ya wanajeshi wa nchi hiyo.
Soma zaidi: UNICEF: Maelfu ya watoto hawana makaazi mashariki mwa DRC
Serikali ya Kigali kupitia msemaji wake Yolande Makolo imetupilia mbali madai ya ripoti hiyo na kusema Rwanda ina uhuru na haki halali ya kutetea eneo na raia wake na sio tu kusubiri hadi kutokee maafa na kuongeza kuwa chimbuko la uwepo wa kundi la M23 linafahamika vyema kuwa ni tatizo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwa nchi hiyo ina lengo la kuutwisha mzigo huo kwa nchi nyengine.
(AP, AFP)