1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Congo kutathmini upya muda wa MONUSCO kuondoka DRC

2 Agosti 2022

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itatathmini upya mpango wa kuondoka kwa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa, kufuatia maandamano yaliyosababisha vifo wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4F1qY
Demokratische Republik Kongo | Goma | Proteste gegen UN
Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Serikali imesema hayo usiku wa kuamkia Jumanne na kudokeza kwamba huenda itauomba ujumbe huo kuondoka mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Serikali imesema raia 36 waliuawa na vilevile walinda amani wanne wa MONUSCO waliuawa wakati wa maandamano hayo ya vurugu. Waandamanaji walikuwa wakiwataka wanajeshi hao wa kulinda amani kuondoka nchini humo kwa sababu wameshindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi kutoka makundi ya wanamgambo ambayo yamekuwa yakiwahangaisha kwa miongo mingi.

"Serikali imeamriwa kuharakisha mkutano na MONUSCO ili kutathminiupya mpango wao wa kuondoka nchini,” tarifa ilisema bila kutoa maelezo zaidi.

Ujumbe wa MONUSCO ambao ulichukua nafasi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwepo 2010, umekuwa ukipunguza idadi ya walinda amani wake kwa miaka. Muda wake wa kudumu nchini humo unatarajiwa kumalizika Disemba. Msemaji wa ujumbe huo hakutoa kauli yoyote ya moja kwa moja kuhusu tarifa hiyo ya serikali.

Waandamanaji nchini DRC waliharibu vitu na kuwasha moto katika majengo ya ujumbe wa MONUSCO.
Waandamanaji nchini DRC waliharibu vitu na kuwasha moto katika majengo ya ujumbe wa MONUSCO.Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walishutumiwa kwa kutumia nguvu kujibu vurugu za waandamanaji, wakati mwingine wakitumia risasi za moto, huku mamia ya waandamanaji wakiwarushia mawe na kuwatupia mabomu ya petroli, kuharibu vitu na kuwasha moto katika majengo ya Umoja wa Mataifa.

Tume ya Congo yabaini maneno ya chuki dhidi ya MONUSCO

Tume ya serikali iliyotumwa kuchunguza yaliyotokea kwenye ghasia hizo, ilibaini kuwa watu 13 walikufa kufuatia makabiliano yaliyotokea mji wa Goma. Wengine 13 wakiwemo walinda amani waliuawa mji wa Butembo na watatu wakauawa eneo la Kanyabayonga, ikulu ya rais imesema.

Waandamanaji wanne waliuawa katika mji wa Uvira wakati wanajeshi walifyatua risasi iliyokata waya wau meme na kuwaangukia.

Baadhi ya waandamanaji nchini Congo wamekuwa wakiwakosoa walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya mashambulizi ya miongo mingi kutoka kwa wanamgambo.
Baadhi ya waandamanaji nchini Congo wamekuwa wakiwakosoa walinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya mashambulizi ya miongo mingi kutoka kwa wanamgambo.Picha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Raia watatu walikufa katika tukio tofauti iliyoripotiwa siku ya Jumapili wakati wanajeshi waliokuwa wakielekea kujiunga na kikosi cha Umoja wa Mataifa walipofyatua risasi katika kituo cha mpakani.

Tume hiyo imeongeza kuwa takriban watu 170 walijeruhiwa, na kuongeza kuwa kulikuwa na matamshi makali kutoka kwa wawakilishi wa makundi ya kiraia dhidi ya Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa ulishutumu vurugu hizo na kuapa kwamba utachunguza madai ya ukiukwaji haki uliofanywa na pande zote kwa ushirikiano wa maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameghadhabishwa na matukio hayo na ametaka "uwajibikaji".

Rais Tshisekedi ataka maafisa waliosababisha maafa waadhibiwe

Kikosi cha UN chakiri kuhusika na ufyatuliaji risasi DRC

Kwenye taarifa yake ya siku ya Jumatatu msemaji wa serikali ya Congo Patrick Muyaya alisema Rais Felix Tshisekedi amemuelezea Guterres kusikitishwa kwake na matendo walinda amani katika kituo cha mpakani na amehimiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya waliohusika.

Kulingana na tovuti ya MONUSCO, ujumbe huo ulikuwa na zaidi ya wanajeshi 12,000 na polisi 1,600 waliotumwa Congo Novemba 2021, kulingana na tovuti yao. Kwa miaka mingi, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukizongwa na tuhuma za kukiuka haki za binadamu.

Ghadhabu dhidi ya MONUSCO zilizidishwa na ongezeko la mashambulizi ya hivi karibuni kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa kundi la M23 mashariki mwa Congo, na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao.

Mashambulizi yanayofanywa na kundi hilo linalohusishwa na lile linalojiita Dola la Kiislamu IS, yamekuwa yakiendelea licha ya hali ya dharura ambayo imekuwepo kwa muda wa mwaka mmoja sasa huku operesheni ya kijeshi ikifanywa na jeshi la Congo kwa ushirikiano na Uganda.Zaidi ya makundi 120 ya wanamgambo yako mashariki mwa Congo.

(RTRE, AFPE)