UN, Saudia zaonya kuhusu operesheni ya Israel huko Rafah
10 Februari 2024Saudi Arabia, imesema siku ya Jumamosi kwamba operesheni ya jeshi la Israel inayopangwa kuendeshwa huko Rafah itasababisha "janga la kibinadamu" huku ikilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.
Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya ufalme huo, imeeleza wazi kuwa Saudia inapinga na kulaani vikali hatua hiyo, huku ukionya juu ya kile walichokiita "athari za mashambulizi ya kuvizia" huko Rafah na kitendo cha kuwahamisha kwa mabavu raia wa Palestina.
Soma pia: Israel yapanga kufanya operesheni ya ardhini mjini Rafah
Taarifa hiyo ya Saudia imesisitiza: "Ukiukwaji huu unaondelea wa sheria za kimataifa za kibinadamu, unaonyesha ulazima wa kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama ili kuizuia Israel kusababisha maafa ya kibinadamu."
Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliamuru jeshi lake kujiandaa kuwahamisha raia kutoka Rafah kabla ya operesheni iliyopangwa ya ardhini dhidi ya kundi Hamas katika mji huo wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wanakoishi Wapalestina zaidi ya milioni moja waliokimbia makazi yao.
Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa na Ujerumani
Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa maisha ya raia wa mji wa Rafah. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres, Stephane Dujarric amesema kile kilicho dhahiri ni kwamba watu hao wanatakiwa kulindwa na kuongeza kuwa wasingependa kuona idadi kubwa ya watu wakilazimishwa kuyahama makaazi yao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya kwamba operesheni hiyo ya Israel katika mji wa mpakani wa Gaza wa Rafah itasababisha "janga la kibinadamu."
Soma pia: UN yahofia usalama wa raia walioko Rafah
Watawala wa Hamas wameonya siku ya Jumamosi kwamba operesheni hiyo ya jeshi la Israel huko Rafah inaweza kusababisha vifo vya "makumi ya maelfu" ya watu katika mji huo ambao umekuwa kimbilio la mwisho kwa Wapalestina waliokimbia makazi yao kufuatia vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.
Kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas, takriban watu 25 wameuawa wakati mashambulizi ya anga ya Israel katika mji wa Rafah usiku wa kuamkia Jumamosi. Hadi sasa idadi ya vifo huko Gaza imefikia watu 28,064.
(Vyanzo: ap/afp/dpa/reuters)