Wapinzani Tanzania walaani kukamatwa viongozi wao
12 Agosti 2024Jeshi hilo liliwatia mbaroni karibu viongozi wote wa ngazi wa juu ya chama hicho waliokuwa wakijiandaa kushriki kongamano kuadhimisha siku ya vijana duniani ambalo lilipanga kufanyika jijini Mbeya.
Hatua hiyo ya kutiwa nguvuni viongozi wa chama hicho pamoja na wanachama wake waliokuwa wameanza kujikusanya kwa kongamano lao, imezua gumzo kubwa huku Chadema ikilinyoshea kidole cha lawama jeshi la polisi pamoja na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.
Wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Makamu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania bara, Benson Kigaila aliita hatua ya kukamatwa viongozi wa chama hicho kuwa ya kionevu na kubinya vyama vya upinzani.
Alisema kwa kufanya hivyo, jeshi hilo linazidi kudhihilisha namna linavyotuhumiwa kukandamiza ustawi wa kidemokrasia na kucheza mchezo wenye sura ya kupendelea upande mmoja.
Viongozi wa chama hichowalikamatwa Jumatatu wakiwa ofisini kwao jijini Mbeya wakati wakijiandaa kukusanyika kwa ajili ya kongamano kuadhimisha siku ya vijana duniani hii leo.
Waliotiwa mbaroni ni pamoja na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania bara, Tundu Lissu, Katibu mkuu John Mnyika, mwenyekiti wa kanda ya nyasa, Joseph Mbilinyi.
Pia, vijana wanaotajwa kufikia 500 waliokuwa wamefunga safari kuelekea mkoani Mbeya kushiriki kongamano hilo nao walitiwa mbaroni. Ama mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyewasili leo asubuhi jijini Mbeya kwa ajili ya kufuatilia hatma ya viongozi wenzake naye alitiwa korokoroni na polisi.
Hadi sasa hakuna taarifa zaidi zilizotolewa na jeshi hilo juu ya kukamatwa kwa viongozi hao, mbali ya taarifa iliyotolewa hapo jana na Kamishna wa operesheni Awadhi Juma aliyetangaza kupiga marufuku kongamano hilo kwa madai ya kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani. Chadema imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya hatma ya viongozi wake huku ikiwataka wafuasi wake kuwa watulivu.
Kumekuwa na mjadala mkubwa unaendelea kufuatia kitendo cha kukamatwa kwa viongozi hao wa kisiasa hasa katika wakati ambapo vyama vya siasa vimeanza kujipanga kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwezi Novemba na baadaye kufuatiwa na uchaguzi mkuu hapo mwakani.
Mbali ya wanaharakaati kukosoa hatua hiyo, chama cha ACT Wazalendo nacho kimeshutumu kitendo cha kukamatwa kwa wapinzani hao kikisema kinakwenda kinyume na katiba ya nchi inayoruhusu uhuru wa watu kukusanyika.