Tundu Lissu na wenzake waachiwa kwa dhamana
11 Septemba 2023Tundu Lissu na wenzake walikuwa wakijiandaa na ziara ya mkutano wa hadhara katika tarafa ya Loliondo wilaya ya Ngorongoro na polisi wanasema walimkamata kwa sababu hakuwa na kibali cha kufanya mkutano huo wa hadhara.
Tundu Lissu aliwahutubia maelfu ya wananchi tarafa ya Loliondo mwishoni mwa juma lililopita baada ya kutoka wilaya ya Mugumu, Serengeti mkoani Mara, ikiwa ni mwendelezo wa chama cha Chadema wa kuyafikia maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa kufanya mikutano ya hadhara.
Baada ya mkutano huo Lissu na ujumbe wake walianza kuelekea katika tarafa ya Ngorongoro kwa ajili ya mkutano mwingine wa hadhara ndipo walipozuiwa na jeshi la polisi kwa madai kuwa hawakuwa na kibali cha kufanya mkutano huo. Walipelekwa katika kituo cha polisi mkoani Arusha kaskazini mwa Tanzania na wakaachiwa kwa dhamana Jumapili usiku.
Lissu alinukuliwa akisema "Haya ni makosa ya kisiasa. Hawawezi kuzijibu hoja ambazo tumezizungumza kuhusiana na wanachi wa Ngorongoro kuondolewa. wanajaribu kutumia sheria za jinai ili kuficha aibu ya wao kushindwa kujibu hoja zinazohusiana na serikali kujaribu kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro.."
Taarifa ya maandishi ya jeshi la polisi mkoani Arusha iliyotolewa na kamanda wake Justine Maseje inaeleza kwamba inamshilikilia Lissu pamoja na wenzake watatu kwa mahojiano kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isivyo halali pamoja na kuwazuia askari polisi kutekeleza majukumu yao na kwamba baada ya mahojiano, taratibu nyingine za kipolisi zitafuata.
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X mwenyekiti wa taifa wa Chadema Freeman Mbowe, alilaani kukamatwa kwa Lissu na wenzake, akisema kwa sasa chama chake kina hofu na usalama wa viongozi na wanachama wake.
Tuhuma zinazomkabili Tundu Lissu na wenzake zipo chini ya kifungu cha sheria cha 74 cha sheria ya jinai ya Tanzania ambapo pamoja na mambo mengine, kizuia mikusanyiko isiyokuwa na kibali cha polisi. Lissu na wenzake walitakiwa kuripoti leo polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Hili ni juma la tatu la ziara ya CHADEMA katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ambapo chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara.