1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganiaji uhuru Kenya wamtaka Mfalme Charles kuomba radhi

31 Oktoba 2023

Mfalme Charles III wa Uingereza na mkewe, Malkia Camilla, wameanza ziara yao ya kiserikali ya siku nne nchini Kenya, koloni la zamani ambalo wapiganiaji uhuru wanataka ufalme huo kuomba radhi kwa mateso waliyopitia.

https://p.dw.com/p/4YFhg
Waandamanaji wakionesha hasira zao dhidi ya ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Kenya.
Waandamanaji wakionesha hasira zao dhidi ya ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Kenya.Picha: Luis Tato/AFP

Mfalme Charles anakabiliwa na miito ya kumtaka aombe radhi kuhusiana na historia ya umwagaji damu uliosababishwa na ukoloni wa nchi yake, Uingereza.

Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 katika taifa la Kiafrika na Jumuiya ya Madola tangu alipovishwa taji la ufalme mwezi Septemba 2022 baada ya kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth II.

Soma zaidi: Mfalme Charles III ziarani Kenya

Ulimwengu wamuaga Malkia Elizabeth II

Mfalme Charles na mkewe, Camilla, walikaribishwa katika hafla rasmi asubuhi ya Jumanne (Oktoba 31) na Rais wa Kenya William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Ruto aliisifu ziara hiyo akisema ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Hata hivyo, alisema anatambua mambo machungu zaidi ya uhusiano wa kihistoria kati ya Uingereza na Kenya.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inajiandaa kuadhimisha miaka 60 ya uhuru kutoka kwa Uingereza Desemba mwaka huu.