1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapi zinakwendea fedha za kupambana na COVID-19 Afrika?

5 Mei 2020

Tayari Afrika imeanza kupokea misaada ya kifedha kutoka taasisi za kifedha za kimataifa kukabiliana na janga la COVID-19 kwa kuwa uchumi wake tayari uko taabani, lakini swali kubwa ni wapi zinakwenda fedha hizo?

https://p.dw.com/p/3bnD8
Nigeria Abuja | Coronavirus | Jack Ma Hilfsgüter
Picha: Getty Images/AFP/K. Sulaimon

Hivi karibuni Ujerumani iliahidi kuipa Nigeria takribani euro milioni tano na nusu kupitia Mfuko wa Masuala ya Kibinaadamu wa Nigeria kama sehemu ya msaada wa kukabiliana na janga la COVID-19, wiki moja baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza kwamba tayari taifa hilo la magharibi mwa Afrika lilishapokea euro nyengine milioni moja na laki mbili kutoka Umoja wa Ulaya kwa makusudi hayo hayo.

Wakfu wa mwimbaji wa Kimarekani, Rihanna, ulitangaza mwezi Machi kwamba utaipa Malawi kitita cha dola milioni 5 na katikati ya mwezi uliopita, Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia kwa pamoja walitangaza nafuu ya madeni kwa mataifa 19 masikini zaidi barani Afrika. 

Kwa ujumla, kuna matangazo na ahadi nyingi mno kiasi cha kwamba sasa hakuna anayejuwa undani wa chochote. Hili ni jambo ambalo wanaharakati vijana barani Afrika wanataka kulibadilisha. Wakitumia hashtag #FollowCovid19Money, yaani fuatilia fedha za COVID-19, wanataka kuhakikisha kuwa kuna uwazi kwenye usimamizi wa fedha za kupambana na virusi vya korona kote barani Afrika, kuanzia Gambia hadi Zimbabwe.

Wanataka huu uwe mjadala kwenye vipindi vya redio na midahalo ya wazi, anasema Hamzat Lawal, mwasisi wa shirika lisilo la kiserikali la Connected Development, CODE, nchini Nigeria na pia mwanzilishi wa hashtag ya #FollowCOVID19Money. 

"Tuna hakika kwamba ili kupata imani na uungaji mkono wa umma, lazima tuwashajiishe raia kuhakikisha kuna uwazi na uwajibikaji. Baada ya kuomba ufadhili kwa sekta za umma na binafsi, tuligunduwa kwamba serikali sio ziwe zinazungumzia msaada huo, lazima ziweke bayana ni namna gani fedha hizi zimetumika kwa maslahi ya umma." Anasema Hamzat.

Senegal Dakar | Coronavirus | Jack Ma Hilfsgüter
Maafusa wa usalama wa Senegal wakisimamia shehena ya madawa na vifaa vya kukabiliana na COVID-19 iliyowasili kutoka China.Picha: Getty Images/AFP/S Souici

Malawi kama Nigeria

Sharon Kalima wa Malawi pia hataki kuona fedha hizi zikiyeyuka. Akiwa msimamizi wa programu kwenye Kituo cha Sanaa za Afrika na kiongozi wa Vuguvugu la Kufuatilia Fedha za COVID-19 nchini mwake, anafahamu kuwa taifa lake ni miongoni mwa mataifa masikini kabisa duniani, lakini anajuwa pia umasikini huo hautokani na ukosefu wa fedha.

"Malawi ni miongoni mwa mataifa masikini kabisa duniani, lakini ukiangalia hali ilivyo, unaweza kuona kwamba sisi si masikini kwa kuwa hatuna rasilimali. Serikali yetu imejaa ufisadi. Hata tukipata fedha, mathalan kutoka Benki ya Dunia, zitafanyiwa ubadhirifu na maafisa wa serikali," anasema mwanaharakati huyo.

Mfano mzuri wa haya anayoyazungumzia Sharon ni pale mawaziri wa serikali walipokana bungeni kupokea kitita cha fedha za kupambana na COVID-19, lakini baadaye ikafahamika kuwa kupitia vikao vya kuomba fedha hizo, mawaziri hao walijitengea kwacha laki nne na nusu kwa mtu kwa siku, ilhali wahudumu wa afya wakilipwa mshahara wa kwacha elfu sitini kwa mwezi mzima. 

Haya yanazifanya tawala za Afrika siziaminike kwenye kukabidhiwa fedha za kupambana na COVID-19 bila ya kusimamiwa kwa jicho kali la umma, wanasema wanaharakati hawa.