Wanne wafa kwa mkanyagano Siku ya Mashujaa Kenya
20 Oktoba 2023Rais Ruto alizinduwa mpango mpya wa huduma ya afya kwa wote uitwao "Afya Nyumbani" wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika mjini Kericho siku ya Ijumaa (Oktoba 20).
Uzinduzi huu unafuatia hatua ya rais huyo kuidhinisha sheria nne mpya, ambazo zingelitumika kuendesha shughuli za afya kote nchini.
Soma zaidi: Kenya yasaka mikopo zaidi kutoka China
Ruto alisema serikali yake "imetenga shilingi bilioni tatu kila mwaka kwa ajili ya mpango huu."
Serikali ya Kenya inasema inatilia mkazo kuzuia magonjwa na vile vile kuwapa nafasi Wakenya wote kuchangia mfumo mpya wa afya.
"Wahamasishaji wa afya 100,000 watakaotekeleza mfumo huu mpya wameshapewa vifaa vya matibabu, na watapewa simu za kisasa kuwawezesha kufuatilia wagonjwa, kuweka rekodi na kuwasiliana na wizara husika kwa haraka panapokuwa na uhaba wa madawa au matatizo yoyote." Alisema Rais Ruto.
Awali kumekuwa na matukio ya wizi wa madawa kutoka kwenye vituo vya afya, hali iliyokuwa inawafanya wagonjwa kukosa madawa kwa muda mrefu.
Siasa yaingia kati kwenye maadhimisho
Hata hivyo, viongozi waliohudhuria kwenye sherehe hiyo hawakusita kuibua masuala ya kisiasa, ikizingatiwa kuwa sherehe yenyewe ilifanyika katika ngome ya Rais Ruto.
Naibu Rais Rigathi Gachagua alichukau fursa hiyo kuonesha nguvu za serikali yao, akiwakosowa wapinzani kwa kutokuwa na mawazo ya kimaendeleo.
Soma zaidi: Ruto ataka uwekezaji zaidi wa China barani Afrika
Sherehe hiyo ilivutia umati mkubwa wa watu, baadhi yao wakilala nje ya uwanja wa sherehe ilimradi wasikose nafasi.
Msongamano wa asubuhi ulisababisha mkanyagano na polisi wamethibitisha kuwa watu wanne walifariki dunia na zaidi ya kumi kujeruhiwa kwenye mkanyagano huo.
Imetayarishwa na Wakio Mbogho/DW Nakuru