Wanamgambo 3,000 wa IS wajisalimisha
13 Machi 2019Kiasi ya wapiganaji 3,000 wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS wamejisalimisha kutoka kwenye ngome yao ya mwisho ya Baghouz mashariki mwa Syria kwa vikosi vya Kikurdi, baada ya kuanza tena mashambulizi ya anga na makombora.
Wanamgambo wa Kikurdi wa Syrian Democratic Forces, SDF, wanaoungwa mkono na Marekani, kwa wiki kadhaa wamekuwa wakijaribu kuwasambaratisha kabisa wapiganaji wa IS, lakini uwepo wa idadi kubwa ya wanaume pamoja na wanawake na watoto ulisababisha mashambulizi hayo kufanyika taratibu.
Tangu Jumapili iliyopita mashambulizi ya anga yameendelea Baghouz kwa siku tatu mfululizo na kuwaua wapiganaji kadhaa wa IS, hali ambayo pia iliwashinikiza wengine kujisalimisha pamoja na familia zao. Mamia wengine walijisalimisha hapo jana.
Msemaji wa SDF, Mustafa Bali, amesema idadi ya wapiganaji wa IS waliojisalimisha tangu Jumatatu jioni imefikia 3,000 na kwamba wanawake watatu na watoto wanne kutoka jamii ya wachache ya Yazidi pia wameokolewa.
SDF hapo jana ilisimamisha mashambulizi hayo kwa muda katika kijiji kinachodhibitiwa na IS cha Baghouz, mashariki mwa Syria ili kuruhusu raia kuondoka kwenye kijiji hicho na kujisalimisha. Siku ya Jumatatu muungano huo ulifanya mashambulizi 20 ya anga dhidi ya wanamgambo hao, na kuharibu magari yaliyokuwa na silaha, alisema Bali.
Kamanda wa kikosi cha wapiganaji wa SDF aliyetambulishwa kwa jina la Shareef alipozungumza na shirika la habari la AFP hapo jana alisema "Wapiganaji wametokea maeneo mbalimbali. Wameonyesha utayari mkubwa hii leo. Tumewasili leo na sasa wanapumzika. Mungu akipenda, tutashambulia Baghouz leo jioni."
Kamanda wa vikosi vya muungano unaoongozwa na Marekani Ali Cheir ameliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi hivyo vinajiandaa kuvamia kijiji hicho. Amesema, wanadhani bado kuna mamia ya wanamgambo waliojificha. SDF mara kadhaa ilisitisha mashambulizi katika kijiji hicho cha Baghouz kutokana na idadi kubwa ya raia, wengi wao wakiwa ni wake na watoto wa wanamgambo wa IS.
Takriban watu 60,000 wameondoka Baghouz tangu mwezi Disemba, hii ikiwa ni kulingana na shirika linaloangazia haki za binadaamu la Syria lenye makao yake Uingereza. Shirika hilo linakadiria kuwa asilimia 10 ya raia hao huenda wakawa ni wanamgambo wa IS.
Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu wanaokimbia Baghouz na kuingia katika kambi inayosimamiwa na Wakurdi, maalumu kwa wakimbizi wa ndani ilikuwa ni ndogo ilikilinganishwa na wiki iliyopita, lakini ikisema wanafika wakiwa na hali mbaya sana tofauti na awali. Shirika la chakula la Umoja huo, nalo kwa upande wake limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya chakula kwa watu wanaokimbilia kwenye kambi hiyo ya Al-Hol.
Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo