Wanajeshi Niger watangaza baraza la mawaziri
10 Agosti 2023Usiku wa kuamkia leo, utawala wa kijeshi nchini Niger ulitangaza kupitia televisheni ya taifa mawaziri 21 wanaounda serikali mpya ya nchi hiyo.
Hatua hiyo imetangazwa wakati Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Ukanda wa Afrika Magharibi, ECOWAS ikikutana kwa mkutano wa kilele wenye azma ya kufikia maakubaliano juu ya hatua za kuchukuliwa kuelekea Niger.
Mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa Jumuiya ya ECOWAS unafanyika katika mji mkuu wa Nigeria Abuja na huenda ukatowa mwelekeo kuhusu mkwamo uliopo nchini Niger.
Viongozi hao wanatarajiwa kukubaliana kuhusu hatua zitakazofuata kuelekea mapinduzi ya kijeshi nchini Niger,hatua ambazo zinatajwa huenda zikajumuisha uingiliaji kati wa kijeshi,jambo ambalo mmoja wa maafisa wa jumuiya hiyo ameshasema itakuwa ni suluhisho la mwisho kabisa endapo njia zote zitashindikana.
Serikali mpya yatangazwa
Hata hivyo ndani ya Niger kwenyewe usiku wa kuamkia leo Alhamisi mtu aliyetajwa kuwa katibu mkuu wa serikali alitangaza majina kupitia televisheni ya watu waliotajwa kuteuliwa mawaziri lakini katibu mkuu huyo hakutangaza mipango mingine yoyote zaidi kupitia tukio hilo.
Serikali iliyotangazwa ni nusu ya idadi ya serikali iliyokuwepo hapo awali. Viongozi wa Jumuiya ya ECOWAS wamewataka wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger wamrudishe madarakani rais Mohammed Bazoum lakini mpaka sasa viongozi wa mapinduzi hayo ya kijeshi wamekataa kuachia madaraka licha ya Jumuiya hiyo kutoa kitisho kwamba inaweza kutumia nguvu kurudisha demokrasia katika taifa hilo.
Tangu Mapinduzi ya Julai 26 yaliyozusha mshutuko katika ukanda huo , wanajeshi wa Niger wameonesha kushikilia msimamo mkali wa kukataa mazungumzo na juhudi zozote za kidiplomasia na hata kwenda mbali zaidi ya kupuuza muda wa mwisho waliowekewa na ECOWAS wa Agosti 6 wa kutakiwa kumrudisha madarakani rais Bazoum.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amezungumzia wasiwasi wake kuhusu Bazoum na familia yake baada ya chama chake kuripoti kwamba wanashikiliwa katika makaazi ya rais,kukiwa hakuna huduma ya umeme wala maji ya bomba,na kwamba pia amekaa siku kadhaa bila ya chakula.
Mkutano wa Abuja utakuja na maazimio gani?
Mkutano wa Abuja kwahivyo unafuatiliwa kwa karibu na hasa kutazama utakuja na maazimio yapi.Wajumbe wa rais wa Nigeria na ambaye ni mwenyekiti wa ECOWAS,Bola Tinubu jana Jumatano walikutana na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi mjini Niamey,na kutowa mwanga wa matumaini ya mazungumzo baada ya timu nyingine za awali za wajumbe kukataliwa.
Hali yoyote ya mapigano inaweza kusababisha ukosefu mkubwa wa uthabiti katika ukanda wa Afrika Magharibi, ambako uasi wa muda mrefu wa makundi ya itikadi kali yamekuwa yakiendesha hujuma na kusababisha mamilioni ya watu kuachwa bila makaazi pamoja na mgogoro mkubwa wa njaa.
Tukumbushe kwamba mapinduzi nchini Nigeri yalisababishwa na hali ya ndani ya kisiasa lakini mgogoro huo umebadilika na kuwa suala la kimataifa linalozihusisha nchi nyingine huku jumuiya ya ECOWAS, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zikiwatia kishindo makanda wa kijeshi wa Niger kuachia madaraka. Na upande wa pili Mali na Burkina Faso zikiapa kuwakingia kifua wanajeshi waliotwaa madarakani Niger.