1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wa hali ya hewa waanza maandamano makubwa

Angela Mdungu
15 Septemba 2023

Maelfu ya wanaharakati wa mazingira, wameanza maandamano leo, wakitoa wito wa kukomesha matumizi ya mafuta ya visukuku, wakati dunia ikikabiliwa na hali mbaya ya hewa pamoja na na joto kali.

https://p.dw.com/p/4WOHV
Maandamano ya wanaharakati wa mazingira
Maandamano ya wanaharakati wa mazingiraPicha: Markus Schreiber/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Maandamano hayo yanayoratibiwa na baadhi ya mashirika ya ndani na makundi yanayoongozwa na vijana likiwemo vuguvugu la "Fridays For Future" chini ya mwanaharakati Greta Thunberg, yanafanyika kwa siku tatu kwenye zaidi ya miji 100 kote duniani.

Sehemu ya maandamano hayo imefanyika katika mji wa Quezon huko Ufilipino ambako wanaharakati walijilaza nje ya Idara ya Mazingira na Rasilimali Asilia, wakiwa wameshika mabango yanayotaka nishati ya visukuku zikiwemo makaa na gesi asilia zisitumike tena.

Soma zaidi: Wanaharakati wa mazingira kuandamana nchi zaidi ya 50

Nako nchini Indonesia, nje ya ofisi ya Wizara ya Nishati na Rasilimali za Madini zilizo mjini Jakarta, wanaharakati wameandamana wakiwa pia wameshikilia mabango yanayotaka matumizi ya nishati zinazosababisha uchafuzi wa hali ya hewa yakomeshwe.

Maandamano mbele ya Kasri la Mfalme wa Sweden

Kwa upande wa Sweden, maandamano kama hayo yamefanyika kwa waandamanaji kukusanyika mbele ya jengo la bunge, umbali mfupi kutoka katika Kasri la kifalme ambako Mfalme wa Sweden Carl wa kumi na sita Gustaf alikuwa akisherehekea miaka 50 tangu alipotawazwa kushika wadhifa huo.

Maandamano ya wanaharakati wa mazingira
Maandamano ya wanaharakati wa mazingira Picha: Markus Schreiber/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Maandamanohayo ya wanahali ya hewa yanafanyika wakati dunia ikikabiliwa na majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kimbunga Idalia kilichotokea kusini mashariki mwa Marekani, mvua kubwa iliyoipiga New Nelhi, India ni baadhi ya matukio yaliyotokana na mabadiliko hayo.

Katika miaka ya hivi karibuni, wanaharakati wa mazingira wamekuwa wakiratibu maandamano kama hayo kote duniani kote, kutaka hatua za haraka zichukuliwe na viongozi wa serikali za dunia ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Maandamano mengine makubwa zaidi yamepangwa kufanyika Jumapili mjini New York ambapo mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa utafanyika.