Wanaharakati wataka serikali ikomeshe mauaji ya wanawake
6 Septemba 2024Mwanariadha Rebecca Cheptegei alifariki dunia jana, siku nne baada ya mpenzi wake kumwagia petroli na kumchoma nyumbani kwake magharibi mwa Kenya. Mwanariadha huyo ni wa tatu wa kike kuuawa nchini Kenya tangu mwaka 2021.
Mwanzilishi wa shirika la Usikimye linalopambana na ukatili wa kijinsia Njeri Migwi amesema ukatili mwingi wa kijinsia hauchukuliwi kuwa ni uhalifu na hivyo kuitaka serikali kuwa na msimamo na kuchukua hatua.
Soma pia: Mwanariadha wa Uganda afariki baada ya mpenzi kumchoma moto
Kumeibuka hofu juu ya ongezeko la visa vya ukatili dhidi ya wanariadha wa kike nchini Kenya. Cheptegei ni mwanariadha wa tatu kuuawa tangu Oktoba 2021.
Mwaka 2022, wanawake 725 walikufa nchini Kenya katika mauaji yanayohusiana na ukatili wa kijinsia, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2015.