Wanadiplomasia wa China na Japan wakutana kwa mazungumzo
25 Novemba 2023Wanadiplomasia wakuu kutoka Japan na China wamekutana kwa mazungumzo leo Jumamosi huku wakijaribu kusuluhisha mizozo kati ya mataifa hayo mawili ikiwa ni pamoja na marufuku ya China kuhusu uuzaji wa bidhaa za baharini za Japan.
Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amekutana na yule wa Japan Yoko Kamikawa katika mji wa mwambao wa Korea Kusini wa Busan ambako wanadiplomasia wakuu wa China, Japan na Korea Kusini wanatarajiwa kukutana kesho ili kujadili changamoto za kikanda na kimataifa.
China ilichukua hatua hiyo baada ya kinu cha nyuklia cha Fukushima kuanza mnamo Agosti 24, kumwaga baharini taka za nyuklia zisizokuwa na mionzi. Japan imekuwa ikijitetea kuwa maji kutoka kinu hicho ni salama zaidi kuliko viwango vilivyowekwa kimataifa, madai yaliyopingwa na Beijing.