1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa Gaza wapindukia 23,000

8 Januari 2024

Idadi ya watu waliouawa tangu Oktoba 7 kwenye mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza imepindukia 23,000, huku kamanda wa ngazi za juu wa kundi la Hizbullah akiuawa kusini mwa Lebanon na kuongeza uwezekano wa vita.

https://p.dw.com/p/4az0f
GAZA Al Jazeera-Korrespondent Wael Al-Dahdouh nimmt während der Trauerfeier im Herzen des Nuseirat-Lagers im Gazastreifen herzzerreißend Abschied von seiner Frau, seinem Sohn und seiner Tochter
Mwandishi wa habari wa Al Jazeera, Wael Al-Dahdouh (kulia) kwenye maziko ya mtoto wake, Hamza (pia mwandishi wa habari wa kituo hicho), aliyeuawa siku ya Jumapili (Januari 7) na mashambulizi ya Israel katika kitongoji cha Khan Younis, Ukanda wa Gaza.Picha: Middle East Images/ABACA/IMAGO IMAGES

Siku ya Jumatatu (Januari 8), madaktari, wagonjwa na wakimbizi wa ndani waliripotiwa kukimbia kutoka hospitali kuu katikati mwa Ukanda wa Gaza wakati mapigano makali kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Kipalestina yakikaribia eneo hilo, kwa mujibu wa mashahidi.

Kuipoteza hospitali hiyo kutakuwa pigo jengine kubwa kwenye mfumo wa afya ambao tayari umeshasambaratishwa na miezi mitatu ya makombora na mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Ukanda huo. 

Soma zaidi: Kifo cha kiongozi wa Hamas: Unachohitaji kujua kuhusu Hezbollah

Wafanyakazi wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka na wa mashirika mengine ya misaada walilazimika kuondoka kwenye Hospitali ya Mashahidi wa Al-Aqsa katika kitongoji cha Deir al-Balah wakisema maisha yao yako hatarini. 

Wasiwasi na fadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamejihifadhi kwenye hospitali hiyo uliwafanya kukimbilia upande wa kusini mwa Gaza, ambako hata huko nako kumekuwa kukishuhudia mashambulizi makali na vifo vya raia kila uchao.

Waliouawa Gaza wapindukia 23,000

Maiti na majeruhi zaidi wamepokelewa kutoka eneo la Khan Younis, ambako wizara ya afya ya Gaza inasema asubuhi ya leo watu 73 waliuawa na wengine 99 kujeruhiwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Hali baada ya mashambulizi ya Israel katika kijiji cha Naqoura kusini mwa Lebanon.
Hali baada ya mashambulizi ya Israel katika kijiji cha Naqoura kusini mwa Lebanon.Picha: Ali Hashisho/Xinhua/picture alliance

Wizara hiyo ya afya imeongeza kuwa kufikia mchana wa leo, jumla ya Wapalestina 23,084 walikuwa wameshauwa kwenye Ukanda huo huku wengine 58,926 wakijeruhiwa tangu Oktoba 7. 

Soma zaidi: Israel, Hizbullah washambuliana tena

Hapo jana, jeshi la Israel liliwauwa waandishi wa habari wawili wa mashirika ya AFP na Al-Jazeera ikidai kuwa walilengwa wakiwa kwenye gari lililokuwa likitumiwa na magaidi.

Hamza Dahdouh na Mustafa Thuria waliuawa kusini mwa Gaza wakiwa magharibi mwa kitongoji cha Khan Younis, kwa mujibu wa kituo cha Al Jazeera.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari, CPJ, yenye makao yake nchini Marekani, kufikia Jumatatu ya leo, waandishi 79 wameshauawa tangu Oktoba 7 kwenye mzozo huu.

Miongoni mwao ni Wapalestina 72, Waisraeli wanne na Walebanon watatu. Hata hivyo, wizara ya afya ya Gaza inasema waandishi wa habari waliokwishauawa ni zaidi ya 100.

Kamanda wa Hizbullah auawa

Hayo yanajiri wakati ripoti kutoka Beirut zikisema kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yamemuua kamanda wa ngazi wa juu wa kundi la Hizbullah kusini mwa Lebanon. 

Libanon | nach Explosion in Dahiyeh
Mfanyakazi wa kikosi cha ulinzi wa raia akitafuta mabaki ya miili kufuatia shambulizi la kombora dhidi ya gari alilokuwamo naibu kiongozi wa Hamas mjini Beirut, Saleh Arouri, siku ya tarehe 3 Januari 2024 nchini Lebanon.Picha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Afisa mmoja wa usalama wa Lebabon ameyaambia mashirika ya habari ya kimataifa kuwa Wissal al-Tawil aliuawa asubuhi ya leo akiwa kwenye gari lake. 

Soma zaidi: Vita vya Israel vyahofiwa kusambaa maeneo mengine

Hizbullah imethibitisha kutokea kwa kifo hicho, ingawa haijatoa ufafanuzi zaidi.

Tawil ni afisa wa kwanza wa ngazi za juu kwenye kundi Hizbullah kuuawa tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 kusini mwa Israel yaliyochochea vita vinavyoendelea sasa. 

Tangu wakati huo, Hizbullah na jeshi la Israel wamekuwa wakishambuliana hapa na pale, lakini mauaji haya na yale ya wiki iliyopita dhidi ya naibu kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas yaliyofanyika kwenye ngome ya Hizbullah mjini Beirut yanaangaliwa na wengi kama hatua za mwisho mwisho kuingia kwenye vita vikubwa vya moja kwa moja kati ya Israel na Lebanon.

Vyanzo: Reuters, DPA