1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Israel vyahofiwa kusambaa maeneo mengine

22 Oktoba 2023

Khofu ya kusambaa kwa vita vya Israel na Wapalestina kote Mashariki ya Kati imeongezeka, huku Marekani ikipeleka zana zaidi za kivita na Israel ikiendelea kuyashambulia maeneo ya Gaza, Ukingo wa Magharibi na Syria.

https://p.dw.com/p/4XsF4
Mashambulizi ya Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili ya 22 Oktoba 2023.
Mashambulizi ya Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili ya 22 Oktoba 2023.Picha: Said Khatib/AFP

Israel iliongeza muda na eneo la mpango wake wa kuwahamisha wananchi katika eneo la kaskazini linalopakana na Lebanon, siku ya Jumapili (Oktoba 22) wakati vita na wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Hizbullah vikiongezeka. 

Israel ilisema ndege zake zilishambulia maeneo ya wanamgambo wa Hizbullah nchini Lebanon siku ya Jumamosi na kwamba mmoja wa wanajeshi wake alilengwa na kombora katika mapigano ya eneo la mpakani.

Soma zaidi: Israel yaionya Hizbullah kuiingiza Lebanon vitani

Kwenye mapigano hayo, kundi la Hizbullah linaloungwa mkono na Iran lilisema wapiganaji wake sita waliuliwa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilifahamisha kwamba waziri wake, Antony Blinken, alikuwa amemtahadharisha kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati kwamba wananchi wake wangeliathirika ikiwa nchi hiyo ingelijiingiza kwenye vita hivi. 

Israel yashambulia Syria

Makombora ya Israel yalilenga pia viwanja vya ndege katika miji ya Damascus na Aleppo katika nchi jirani ya Syria na kuharibu kabisa shughuli za viwanja hivyo huku raia mmoja akiuawa, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Syria. 

Wapalestina wakikaguwa madhara ya mashambulizi ya Israel kwenye kiunga cha Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili (Oktoba 22).
Wapalestina wakikaguwa madhara ya mashambulizi ya Israel kwenye kiunga cha Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumapili (Oktoba 22).Picha: Said Khatib/AFP

Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema nchi yake ingelipeleka zana zaidi za kivita katika Mashariki ya Kati kuiunga mkono Israel na kuimarisha uwezo wake wa kijeshi katika ukanda huo kufuatia kile kilichotajwa kama kuongezeka mivutano iliyosababishwa na Iran pamoja na vikosi inavyoviunga mkono. 

Soma zaidi: Jee Israel na Chama cha Hamas watasitisha kweli mapigano?

"Mifumo ya kisasa ya ulinzi ikiwemo mfumo wa anga wa kuzuia makombora wa Patriot utapelekwa katika eneo hilo  na wanajeshi zaidi watawekwa tayari." Alisema waziri huyo wa ulinzi wa Marekani, muungaji mkono mkubwa wa Israel. 

Zaidi ya 50 wauwa Gaza

Zaidi ya Wapalestina 50 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofanywa usiku wa kuamkia Jumapili katika Ukanda wa Gaza. 

Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi (Oktoba 21.)
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi (Oktoba 21.)Picha: Abed Khaled/AP Photo/picture alliance

 Siku ya Jumamosi (Oktoba 21), wizara ya afya ya Gaza ilisema mashambulio ya makombora ya kulipiza kisasi ya Israel yameuwa takribani Wapalestina 4,385 wakiwemo watoto, huku zaidi ya watu milioni moja wakiachwa bila makaazi katika Ukanda huo.

Soma zaidi: Yajuwe makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati na Afrika

Israel imekusanya vifaru na wanajeshi wake katika eneo la mpaka wa Gaza  uliojengewa uzio, ikijiandaa kufanya mashambulizi ya ardhini inayodai yataliangamiza kabisa kundi la Hamas. 

Kwa mara nyingine, Israel imetowa onyo kupitia vipeperushi ikiwataka watu waondoke kaskazini na kuelekea kusini mwa Gaza, ikisema tayari watu wanaokadiriwa kufikia 700,000 wameshaondoka kwenye eneo hilo lakini maelfu ya wengine wamebakia.

Hata hivyo, mara kadhaa kumekuwa na mashambulizi ya Israel kwenye maeneo hayo ya kusini inakotaka watu wakimbilie, ambapo mamia ya watu wameuawa.

Misaada yaendelea kuingia Gaza

Wakati huo huo, malori ya misaada kwa ajili ya watu wa Gaza yameanza kuingia kwenye eneo hilo wiki mbili baada ya kuanza kwa mashambulizi ya Israel, huku maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yakishuhudiwa katika miji mbali mbali ya dunia kuanzia London, Barcelona, Los Angeles na kwengineko. 

Baadhi ya magari ya misaada yakiingia kwenye Ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi (Oktoba 21).
Baadhi ya magari ya misaada yakiingia kwenye Ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi (Oktoba 21).Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, ametowa mwito wa kusitishwa vita kati ya Hamas na Israel na kuruhusiwa msaada zaidi wa kiutu kuingia Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi:Israel yazishambulia Palestina, Syria

Akizungumza baada ya sala ya Jumapili katika uwanja wa kanisa la mtakatifu Peter mjini Rome, kiongozi huyo wa kiroho alisema "vita siku zote havishindi isipokuwa vinaharibu misingi ya ubinadamu."

Israel ilianzisha operesheni ya kuizingira kikamilifu na Gaza baada ya wanamgambo wa Hamas kutoka ukanda huo kuvuuka na kuingia kusini mwa Israel  na kufanya mashambulio yaliyouwa Waisrael 1,400, wengi wakiwa raia, shambulio ambalo lilisababisha mshtuko kwa Israel.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW