1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliofukuliwa Shakahola wafikia 211

17 Mei 2023

Shughuli ya ufukuaji miili katika Msitu wa Shakahola pwani ya Kenya imerejea tena baada ya siku mbili za mapumziko, ambapo miili 10 imefukuliwa na kuongeza idadi ya waliokufa kufikia 211.

https://p.dw.com/p/4RUgx
Kenyans seek relatives among starvation cult victims in Malindi
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Wanaume watatu waliokuwa wamefunga wameokolewa wakiwa hali mahututi, watatu hao wamepelekwa hospitali kwa matibabu.

Aidha wanaume wengine wanne wanaosemekana kuwa wasimamizi wa watu wanaofunga msituni shakahola wametiwa mbaroni.

Maafisa walioko msituni wamefichua vifaa vilivyokuwa vinatumika kuyachimba makaburi ya waumini wanaofunga vilivyokuwa vimefichwa.

Hata hivyo shughuli ya ufukuaji huenda ikachukua muda zaidi ikizingatiwa kuwa bado yapo makaburi mengine yaliyotambuliwa msituni ambayo yanasubiri kufukuliwa.

Idadi ya watu walioripotiwa kuwa hawajulikani walipo imefikia watu 610.