Waliofariki katika moto wa nyika Los Angeles wafikia 16
12 Januari 2025Watu 16 wamekufa kutokana na moto mkubwa wa nyika, unaoendelea kuteketeza eneo la mji wa Los Angeles katika jimbo la California nchini Marekani. Watu 11 walikufa katika moto wa Eaton karibu na Pasedena na wengine watano wamefariki katika moto mwingine unaowaka kwenye wilaya ya Pacific Palisades.
Idara ya zimamoto inakadiria kwamba zaidi ya nyumba 5,300 zimeteketea kwa moto katika kitongoji cha Pacific Palisades tangu siku ya Jumanne huku majengo zaidi ya 7,000 yakihofiwa kuchomeka katika eneo la Eaton.
Mkuu wa idara ya zimamoto Antony Marrone ameonya kwamba kitisho cha moto kinasalia kuwa juu kwasababu ya upepo mkali, hali ya hewa na uoto mkavu.
Naye Gavana wa California Gavin Newsom, ameeleza kwamba vikosi vya zima moto kutoka Mexico vimewasili mjini humo kusaidiana na maafisa takribani 14,000 wanaopambana kuudhibiti moto huo.