1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Watu 10 wafa kwa moto wa nyika Los Angeles, Marekani

10 Januari 2025

Watu wapatao 10 wamekufa kutokana moto wa nyika unaoendelea kuuteketeza mji wa Los Angeles, katika jimbo la Carlifonia, Marekani.

https://p.dw.com/p/4p19S
Moto Los Angeles, California
Watu wakikumbatiana baada ya kuhamishwa kufuatia moto mkubwa ulioukumba mji wa Los Angeles, jimboni California, Januari 8, 2025.Picha: David Swanson/REUTERS

Taarifa ya mchunguzi wa kiafya wa jimbo hilo, imesema miili yote inasubiri kutambuliwa kisheria na ndugu zao. 

Mapema jana, Rais Joe Biden alisema kuwa moto huo unaowaka katika eneo la Greater Los Angeles, ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya jimbo hilo la magharibi mwa Marekani. 

Biden amesema watu 360,000 wameondolewa hadi sasa. Hata hivyo, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana. 

Soma pia: Maelfu watumwa kuukabili moto wa nyika California

Kulingana na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto cha Los Angeles, Kristin Crowley, zaidi ya nyumba 5,300 zimeharibiwa katika kitongoji cha Pacific Palisades peke yake tangu siku ya Jumanne. 

Aidha, Takribani majengo 4,000 hadi 5,000 yameungua au kuteketea kabisa katika eneo la Eaton Fire karibu na Pasadena.