1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Walinzi wa rais Yoon wakaidi miito ya kufika mbele ya polisi

4 Januari 2025

Siku moja baada ya kushindwa kumkamata Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani na bunge Yoon Suk Yeol, wakuu wa kitengo chake cha ulinzi wamekataa wito wa kufika mbele ya polisi Jumamosi ili kuhojiwa.

https://p.dw.com/p/4ooUX
Polisi wa Korea Kusini wakiondoka nyumbani kwa rais aliyeondolewa madarakani na bunge baada ya kushindwa kutekeleza waranti wa kumkamata
Wapelelezi wamemuomba kaimu rais kuamuru kitengo cha ulinzi wa rais kuheshimu waranti wa kukamatwa Rais YoonPicha: Kim Hong-Ji/REUTERS

Shirika la habari la Yonhap limesema kitengo cha ulinzi wa rais kimefafanua kuwa mkuu wake Park Chong Jun na naibu wake Kim Seong Hoon hawawezi kuondoka katika nafasi yao, wakati Yoon anahitaji ulinzi wa kila mara kutokana na hali tete inayoendelea kushuhudiwa. Kitengo hicho kinawasiliana na polisi kutafuta tarehe nyingine ya kuwahoji wakuu wake.

Ijumaa, makumi ya wapelelezi walijaribu kwa karibu masaa sita kumkamata Yoon ili ahojiwe kufuatia kutangaza kwake sheria ya kijeshi mapema Desemba. Hata hivyo, zaidi ya maafisa wa 200 wa ulinzi wa rais na jeshi walisimama kwenye msitari kutengeneza ukuta na kushikana mikono na wakawazuia wapelelezi waliofika katika makazi rasmi ya rais huyo mjini Seoul.

Sasa wapelelezi hao wa Ofisi ya Kuchunguza Rushwa kwa mara nyingine wamemuomba kaimu rais Choi Sang-mok, ambaye pia ni waziri wa fedha, kuamuru kitengo cha ulinzi wa rais kuheshimu waranti wa kukamatwa Rais Yoon.