Wakimbizi wajasiriamali nchini Uganda
20 Juni 2023Vijana wakimbizi kutoka Burundi ambao kundi lao la Mirror Group ni maarufu katika kutumbuiza kwenye sherehe na makongamano ya kimataifa.
Ni kutokana na shughuli hii ya kucheza ngoma za kienyeji ndipo wengi wao wameweza kujikimu mahitaji yao ikiwemo kujilipia karo shuleni na kuboresha maisha yao hata kwa maigizo.
Huu ni mfano wa jinsi wakimbizi nchini Uganda wanavyodhihirisha kuwa na matumaini na ndoto chanya kuhusu mustakabali wao licha ya kuwa ugenini.
Bila shaka hiki ni kielelezo cha kauli ya mwaka huu ya siku ya wakimbizi duniani. Ujumbe wa kauli mbiua hii ni kuwa na matumaini licha ya kutokuwa nyumbani ili kuwezesha wakimbizi kuishi katika dunia ambako wanahusishwa katika masuala yote ya maisha ya kawaida bila kubaguliwa.
Fursa sawa kwa wakimbizi ?
Kutokana uhuru na fursa sawa za kushiriki biashara na mafunzo mbalimbali ya stadi za mikono, makundi kadhaa ya wakimbizi wanawake wanashuhudiwa wakiendesha kazi za ushoni na ususi katika mitaa mbalimbali ya Kampala.
Kwa upande wa wanaume, wanatambuliwa pia kuwa washoni na vinyozi stadi. Wanaishi katika mazingira ya matumaini licha ya kuwa hawako nchini kwao ambako ndiko hasa nyumbani kwao. Hali kama hii ndiyo imewaepusha wakimbizi wengi wa kike dhidi ya maovu kama vile ukahaba kama kisingizio cha kujikimu mahitaji.
Wakumbatia mila na desturi za wenyeji
Kwa upande mwingine, wakimbizi wamewavutia wenyeji nchini Uganda kuiga na kumbatia desturi mbalimbali za maisha yao. Miongoni mwa hizo ni mitindo ya mavazi na hata mapishi.
Kwa mfano kitoweo cha sombe sasa ni maarufu miongoni mwa waganda na siku hizi majani ya mmea wa muhogo ni ya thamani kubwa kwa wakulima kuliko hapo awali. Hivi majuzi mawaziri kutoka mataifa ya Mashariki mwa Afrika walizindua mkakati wa kuwa na suluhu la kudumu kwa wakimbizi.
Ukarimu wa Waganda
Wadau katika suala zima la kuwatunza wakimbizi wametambua kwamba kuwahusisha wakimbizi katika maisha ya kawaida ni huwandaa ipasavyo kwa mustakabali wao wakiamua kurudi nyumbani kwao kwa hiari yao au kwenda nchi nyengine.
Kwa msingi huu, wakimbizi hawapaswi kuishi na unyanyapaa, majonzi na majuto kutokana na hali zilizowalazimu kuyakimbia makazi yao.