Wakimbizi Afrika Magharibi na Kati wafikia milioni 14
20 Septemba 2024Kamishna Mkuu wa UNHCR, kanda ya Afrika Magharibi na Kati Abdouraouf Gnon-Konde, amesema idadi hiyo imeongezeka kutoka wakimbizi milioni 6.5 mwaka 2019 hadi milioni 13.7 mwaka 2024.
Idadi ya wakimbizi inatarajiwa kuongezeka
Gnon-Konde amewaambia waandishi habari mjini Abidjan nchini Ivory Coast kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka huu, wanatarajia idadi hiyo kuongezeka kufikia kati ya watu milioni 14 na hata milioni 15 kufikia mwishoni mwa mwaka 2015.
Soma pia:Idadi ya wakimbizi kanda ya Afrika Magharibi na Kati imeongezeka maradufu
Idadi hiyo hata hivyo haijumuisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambapo UNHCR inakadiria kuwa takriban watu milioni saba wamepoteza makazi yao.
Gnon-Konde ameongeza kuwa Chad,mojawapo ya mataifa maskini zaidi duniani, inakabiliwa na hali mbaya sana huku mtu mmoja kati ya watu 17 nchini humo akiwa mkimbizi.
Chad imepokea idadi kubwa ya wakimbizi wa Sudan
Nchi hiyo imewapokea wakimbizi 650,000 waliokimbia nchi jirani ya Sudan tangu vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka mwezi Aprili mwaka 2023.
Kabla ya vita hivyo nchini Sudan, Chad, nchi yenye idadi ya watu milioni 17, ilikuwa tayari inawahifadhi wakimbizi 420,000 wa Sudan.
Kamishna huyo wa UNHCR amesema maelfu ya watu kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria na Cameroon, wote wakikabiliwa na changamoto za kiusalama, pia wamekimbilia nchini Chad.
Usalama katika eneo la Sahel, ambako pia inapatikana Chad, umezorota kwa kiasi kikubwa katika muda wa muongo mmoja uliopita.
Soma pia:Makambi ya wakimbizi Chad yakabiliwa na mzozo wa kiutu
Gnon-Konde anasema huku Mali, Burkina Faso na Niger zikikumbwa na ghasia za makundi ya itikadi kali, kati ya watu milioni 4.5 na 5 wameyahama makazi yao, hasa ndani ya nchi, na kuongeza kuwa wengine walikimbilia nchi za Ghuba ya Guinea, pamoja na Mauritania na kusini mwa Algeria.
Wakimbizi watakiwa kujumuishwa katika mipango ya maendeleo
Huku watu wengi waliokimbia makazi yao wakishindwa kurejea nyumbani, baadhi yao ikiwa ni miongo kadhaa sasa, UNHCR imetoa wito kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi hao kuwajumuisha katika mipango yao ya maendeleo.