1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya watatu waliotoweka wakati wa maandamano waachiwa

20 Septemba 2024

Mashirika ya haki za binadamu nchini Kenya yamesema raia watatu waliotekwa wakati wa maandamano ya vijana wa Gen-Z wameachiliwa, na kuvishutumu vikosi vya usalama kuwashikilia mateka.

https://p.dw.com/p/4ktiN
Themenpaket Afrika Kenia Proteste
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonesha wawili kati ya wanaume hao, wakionekana wenye hofu baada ya kuwachiliwa katika eneo la mbali Alhamisi usiku.

Afisa wa tume ya haki za binadamu ya Kenya, Cornelius Oduor, alithibitisha kuwachiliwa kwa watu hao, na kuongeza kuwa hakuna uthibitisho wa wapi watu hao ambao ni Bob Njagi, Aslam Longton, na kaka yake Jamil Longton walikuwa wanashikiliwa.

Lakini Oduor amesema wanaamini pasina shaka kwamba walichukuliwa na mawakala wa usalama wa Kenya.

Ndugu hao wawili walitupwa kwenye eneo la vijijini nje ya jiji la Nairobi, kulingana na ujumbe wa mtandao wa X uliochapishwa na rais wa chama cha wanasheria nchini Kenya, wakati Njagi alijiwasilishwa kwenye kituo cha polisi cha Tigoni.

Kadhia hiyo imepamba vichwa vya habari nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, baada ya mahakama mjini Nairobi kumtia hatiani naibu mkuu wa jeshi la polisi, Gilbert Masengeli, kwa kosa la kudharau mahakama, kutokana na kushindwa kutokea mahakamani kujibu maswali juu ya kutoweka kwa wanaume hao watatu.

Soma pia: 

Masengeli, ambaye wakati huo alikuwa akikaimu nafasi ya Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, anadai kuwa alishindwa kujitokeza mahakamani kwa sababu alikuwa mbali kwenye majukumu rasmi.

Alipewa muda hadi Ijumaa kuhudhuria mahakamani ili kuepusha kifungo cha gerezani, agizo ambalo amelitekeleza.

Kenya | Mkuu wa zamani wa polisi, Japhet Koome
Aliekuwa mkuu wa polisi Japhet Koome alijiuzulu wadhifa huo kufuatia vifo vya waandamanaji.Picha: AP Photo/picture alliance

IPOA yachunguza malalamiko zaidi ya utekaji

Oduor amesema wanaamini kuachiliwa kwa wanaume hao kumekusudiwa kutoa sababu za mara moja kwa Masengele kupinga hukumu dhidi yake. Mkuu mpya wa jeshi la Polisi, IGP Douglas Kanja, alisema jana kuwa wanaume hao watatu waliotoweka hawakuwa mikononi mwa polisi.

Mamlaka huru ya usimamizi wa polisi, IPOA, imesema ilikuwa inachunguza malalamiko kadhaa ya ukamataji wa kinyume cha sheria na utekaji kufuatia maandamano makubwa ya kuipinga serikali yaliozuka nchini Kenya mwezi Juni.

Zaidi ya watu 60 walikufa wakati wa maandamano hayo, na kupelekea kujiuzulu kwa mkuu wa jeshi la Polisi Japhet Koome.  Visa vya huko nyuma vya utekaji vimesababisha maandamano pia nchini Kenya.

Mnamo Februari 2023, maafisa watatu walihukumiwa vifungo vya kuanzia miaka 24 gerezani hadi kifo kwa mauaji ya kikatili ya wakili wa haki za binadamu Willie Kimani na watu wengine wawili.

Miili yao iliwekwa kwenye magunia na kutupwa katika mto nje ya Nairobi Juni 2016.

Je, Polisi wapewe mafunzo maalumu kukabili maandamano?