Wakazi katika miji inayozingirwa nchini Syria kuhamishwa
29 Machi 2017Miji miwili yenye idadi kubwa ya washia ya al-Foua na Kefraya katika jimbo la kaskazini mashariki la Idlib yenye mafungamano na serikali imezingirwa na wapiganaji wa makundi ya waasi wakati miji inayodhibitiwa na makundi ya waasi ya Zebadani na Madaya iliyoko karibu na mpaka wa Lebanon imezingirwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali.
Mkuu wa shirika hilo la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman amesema zoezi la kuwaondoa watu katika miji hiyo halitaanza hadi April 4 lakini usitishwaji mapigano katika miji hiyo ulianza usiku wa kuamkia leo na kuwa hali hivi sasa ni shwari katika maeneo hayo.
Miji hiyo minne ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 ambapo pia chini ya makubaliano hayo mashirika ya misaada yamekuwa yakisambaza mahitaji kwenye miji hiyo.
Serikali ya Syria inayoungwa mkono kijeshi na vikosi vya Urusi na Iran imefikia makubaliano kadhaa yanayoashiria uhakika wa usalama wa njia kwa makundi ya pande zote mbili yanayohusika na mgogoro huo.
Upinzani nchini Syria wasema hatua hiyo inalenga kuinufaisha zaidi serikali ya Assad
Upinzani nchini Syria unaichukulia hatua hiyo kuwa inalenga kuwaondoa kwa nguvu wapinzani wa Rais Bashar al-Assad kutoka katika miji ya magharibi mwa Syria ambayo kwa kipindi cha miaka sita ya mgogoro wa Syria imekuwa ni mhimili wa utawala wa Rais Assad.
Duru kutoka vyanzo vyenye mafungamano na serikali zimesema utekelezaji wa hatua ya kuondolewa kwa wakazi katika maeneo hayo yaliyozingirwa ulitarajiwa kuanza Aprili 4, kwa kuwaondoa watu 16,000 wanaoishi katika miji ya al-Foua na Kefraya kwa mabadilishano na wanamgambo wa Zabadani na Madaya pamoja na familia zao.
Taarifa hizo hazikuthibitishwa na upande wa upinzani.
Shirika la waangalizi wa haki za binadamu limesema zoezi la kuwaondoa watu kutoka miji ya al-Foua na Kefraya limepangwa kuchukua muda wa siku 60 na kuwa watu watakaoondolewa kwenye miji inayodhibitiwa na waasi watapelekwa Syria Kaskazini.
Makubaliano hayo pia yanahusisha usitishaji mapigano katika maeneo yanayozunguka kusini mwa Damascus pamoja na usambazaji wa misaada ya kiutu na kuachiwa kwa wafungwa 1,500 wanaoshikiliwa na serikali wakihusishwa na vuguvugu la uasi dhidi ya utawala wa Rais Assad.
Zaidi ya watu 320,000 wameuawa na mamilioni zaidi wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mgogoro huo wa Syria ulipoibuka mnamo Machi 2011.
Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE/AFPE
Mhariri: Gakuba, Daniel