1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiTunisia

Wahamiaji 28 waliotelekezwa waokolewa Tunisia

Angela Mdungu
31 Agosti 2024

Shirika la haki za binadamu nchini Tunisia la FTDES limesema, limewaokoa wahamiaji 28 waliokuwa wametelekezwa bila maji wala chakula katika mpaka wa Tunisia na Algeria.

https://p.dw.com/p/4k82J
Serikali ya Uhispania inakadiria kuwa takriban watu 200,000 nchini Mauritania wanaosubiri kwenda visiwa vya Canary
Serikali ya Uhispania inakadiria kuwa takriban watu 200,000 nchini Mauritania wanaosubiri kwenda visiwa vya CanaryPicha: Yousef Murad/AP/picture alliance

Kulingana na shirika la FTDES, kati ya wahamiaji waliookolewa ni wanawake saba, watatu kati yao wakiwa ni wajawazito pamoja na watoto wawili.

Msemaji wa shirika hilo Romdhane Ben Amor amebainisha kuwa, walifanikiwa kuwaokoa kwa msaada wa mamlaka za ndani na walinzi wa taifa ambao waliwapeleka katika kituo cha polisi.

Ben Amor amesisitiza kwamba ni wazi kuwa wahamiaji wengine wako mafichoni na wanahofia kukamatwa na polisi. Wahamiaji hao watahamishiwa katika makazi yaliyo chini ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM

Mapema Alhamisi, shirika hilo liliripoti kuwa waomba hifadhi 42 nchini humo walifukuzwa kutoka mji wa Pwani wa Sfax na kupelekwa katika eneo hilo la mpaka. Tunisia imekuwa kituo kikubwa cha wahamiaji wasio na vibali wanaojaribu kwenda Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.