1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea urais Nigeria waahidi kuyakubali matokeo

13 Februari 2019

Wagombea wawili wakuu wa urais nchini Nigeria wametowa mwito kwa wananchi kutojihusisha na vurugu wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa wiki na kutoa ahadi ya kuyakubali matokeo yatakayotangazwa.

https://p.dw.com/p/3DJci
Wahl in Nigeria
Picha: imago/ZUMA Press

Rais Muhammadu Buhari na Atiku Abubakar wameungana na wagombea wengine kusaini rasimu ya makubaliano ya amani mbele ya waangalizi wa kigeni akiwemo kiongozi wa nchi za Jumuiya ya madola Patricia Scotland.

Waliotia saini makubaliano hayo wamewatolea mwito wafuasi wao kujizuia kujihusisha na vitendo vya vurugu au vitendo vyovyote ambavyo huenda vikachangia kuhujumu mitizamo ya kufanyika uchaguzi huru wahaki na wakuaminika nchini Nigeria.

Kadhalika wametoa ahadi ya kuheshimu matokeo ya uchaguzi utakaokuwa huru.

Wapiga kura wengi ni wanawake na vijana

Wahl in Nigeria
Picha: REUTERS/A. Sotunde

Takriban watu milioni 84 wamejiandikisha kupiga kura siku ya jumamosi katika uchaguzi wa rais na bunge.

Uchaguzi wa magavana wa majimbo pamoja na ule wa mabunge ya majimbo umepangiwa kufanyika mwezi Marchi tarehe 2.

Rais Buhari aliingia  madarakani mwaka 2015 kama kiongozi wa kwanza wa upinzani kuwahi kumuondowa madarakani rais aliyekuweko na mpinzani wake wakati huo Goodluck Jonathan aliyekuwa rais alikubali kushindwa.

Kiongozi huyo wa Nigeria amesema uchaguzi wa mwaka huu ni historia nyingine ukiwa unawashirikisha wanawake wengi zaidi na vijana na kuwa na rikodi ya vyama 91  na zaidi ya wagombea 71 wa urais.

Buhari na Atiku wanapigia upatu utulivu

Präsidentschaftswahl Nigeria Wahlplakate
Picha: DW/K. Gänsler

Buhari ametowa mwito wa kuwepo ushirikiano mkubwa katika siasa ili kusaidia kuyashughulikia masuala ya yanayoikabili nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Kwa upande mwingine Atiku Abubakar aliyewahi pia kuwa makamu wa rais anayesimama kupitia chama cha Peoples Democratic Party PDP anaitaka tume ya uchaguzi na vikosi vya usalama kutoegemea upande wowote.

Tuhuma kwamba rais Buhari na chama chake cha APC wako mbioni kujiweka tayari kuyabadili matokeo au kufanya wizi wa kura ndio suala kuu linalozitawala kampeini za chama cha PDP wakati pia chama hicho kikiwakumbusha wapiga kura kuhusu uongozi wa  Buhari alipokuwa kama mtawala wa kijeshi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri Iddi Ssessanga