Wafanyakazi 280 wa huduma za kiutu waliuawa 2023 - OCHA
19 Agosti 2024Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema siku ya Jumatatu (Agosti 18) kwamba wafanyakazi 280 waliuawa kwenye mataifa 33 katika mwaka 2023.
Hili ni ongezeko la asilimia 137 na zaidi ya mara mbili ya vile hali ilivyokuwa mwaka 2022, ambapo waliouawa walikuwa 118.
Kaimu Mratibu wa Huduma za Dharura wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya, alisema vifo vingi zaidi vya mwaka jana vilitokea kwenye Ukanda wa Gaza katika miezi mitatu ya mwanzo ya mashambulizi ya Israel kwenye ukanda huo yaliyoanza mwezi Oktoba.
"Hali ya kufanya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada kuwa jambo la kawaida na ukosefu wa uwajibikaji ni mambo yasiyokubalika, yasiyoingia akilini na yenye madhara makubwa kwa operesheni za misaada popote yanapotokea. Wenye madaraka lazima wachukuwe hatua za haraka kukomesha mashambulizi dhidi ya raia na hali ya wahalifu kutokuchukuliwa hatua." Aliongeza kaimu mratibu huyo.
Wengi zaidi wauawa Gaza
OCHA ilisema kuwa 123 katika vifo hivyo vilikuwa vya wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ambavyo vilitokana na mashambulizi ya anga ya jeshi la Israel.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba mwaka huu wa 2024 huenda ukawa mbaya zaidi, kwani kufikia tarehe 7 Agosti, tayari wafanyakazi 172 walishauawa.
Soma zaidi: Ujerumani kuanza tena ushirikiano na shirika la Palestina UNRWA
Taarifa iliyotolewa na OCHA ilizugumzia pia jinsi hali inayozidi kuwa mbaya nchini Sudan na Sudan Kusini ilivyochangia ongezeko hilo la idadi ya wafanyakazi wa huduma za kibinaadamu wanaouawa wakiwa kwenye kazi zao.
Wafanyakazi 25 wameuawa nchini Sudan tangu mwezi Aprili 2023 na wengine 34 nchini Sudan Kusini.
Mashirika yawaandikia wanachama UM
Siku ya Jumatatu (Agosti 19), mashirika ya kibinaadamu kote ulimwenguni yaliyaandikia barua mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuyataka yachukuwe juhudi zaidi za kuwalinda wafanyakazi wa misaada wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Huduma za Kibinaadamu.
"Tutaendelea kubakia na kuhudumia kwenye maeneo yenye migogoro kote duniani, lakini hali inatutaka tuwe na msimamo wa pamoja na kutoa wito wa kulindwa wafanyakazi wetu, wahudumu wa kujitolea na raia tunaowahudumia." Ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Soma zaidi:Ujerumani yalaani ongezeko la ghasia dhidi ya UNRWA
Mbali ya Palestina, Sudan na Sudan Kusini, mataifa mengine yaliyomo kwenye orodha ya nchi kumi zenye mauaji mengi zaidi ya wafanyakazi wa misaada ni pamoja na Israel na Syria, ambako wafanyakazi saba waliuawa kwa kila nchi, Ethiopia na Ukraine, ambako wafanyakazi sita waliuawa kwa kila nchi, Somalia iliyokuwa na vifo vitano, na vifo vinne kwa kila moja kati ya Myanmar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Vyanzo: AFP, AP, dpa