Waandamanaji warejea mitaani nchini Kenya
2 Julai 2024Mamlaka ya usimamizi wa polisi ya kujitegemea, IPOA, imeanza kuchunguza matukio yaliyotokea tangu maandamano yaanze kuhusiana na uwajibikaji wa polisi, huku chama cha upinzani cha ODM kikianza kuwafukuza wabunge wake waliouridhia muswada wa fedha wenye utata uliochochea maandamano.
Maandamano ya leo yalifanyika kwenye miji ya Nairobi, Kisii, Nakuru na Mombasa ili kupinga utendaji wa serikali na hali ngumu ya maisha.
Hii ni wiki ya tatu ya maandamano ya kupinga muswada wa Fedha wa 2024 uliozua utata ambao sasa umetupiliwa mbali. Jjini Nairobi polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wanakusanyika kwenye barabara za kuelekea katikati ya jiji.
Wakati huohuo, kulishuhudiwa tukio la ajabu kwenye barabara ya Moi baada ya waandamanaji kubwaga majeneza kumi matupu, wakiwakumbuka waliopoteza maisha wakiwa kwenye maandamano. IPOA kwa sasa inachunguza mauaji ya watu 39 na majeruhi 150 pamoja na wengine 7 waliokamatwa.
ODM chairai serikali kuchukua hatua muafaka dhidi ya waandamanaji
Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa wiki hii kwenye mdahalo wa kitaifa na vyombo vya habari, rais William Ruto alikanusha madai kwamba uongozi wake uliridhia kamatakamata hiyo na kusisitiza kuwa walioshikwa walikuwa wahalifu.
Chama cha upinzani cha ODM, kinadai kwamba watu wasiopungua 50 wamekamatwa na wanazuiliwa na polisi kiyume cha sheria. Kwenye taarifa yao hii leo, katibu mkuu Edwin Sifuna alielezea masikitiko yao na kuitaka serikali kuchukua hatua stahiki.
Kwa upande mwingine, Baraza la Taifa la Makanisa, NCCK, limeurai uongozi wa nchi kusikiliza kilio cha vijana ambao wamechoshwa na hali ngumu ya maisha na kuendelea kuandamana.
Vurugu zimeripotiwa katika miji ya Mombasa na Nakuru, Kisumu na Kisii kulikotokea maandamano ya amani. Duru zinaeleza kuwa polisi wamemkata mtu mmoja aliyedaiwa kuwapiga risasi waandamanaji watatu katika mtaa wa Ganjoni mjini Mombasa.