Waalikwa wa BRICS wasema wataitumia fursa
24 Agosti 2023Viongozi wakuu wa BRICS, inayojumisha Brazil, Urusi,India, China na Afrika Kusini, wamekubaliana katika mkutano wao wa kila mwaka kuzialika Argentina, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa wanachama kamili kuanzia Januari Mosi mwakani.
Soma pia: BRICS yakubali wanachama wapya sita
Rais Xi Jinping wa China, ambaye taifa lake ndilo lenye nguvu zaidi katika kundi la BRICS, amesema kutanuka kwa umoja huo ni ishara ya kujengeka kwa mfumo mpya wa kilimwengu usiotegemea pekee mataifa ya Magharibi:
"Uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea katika utawala wa kimataifa unapaswa kuongezwa, na nchi zinazoendelea zinapaswa kuungwa mkono katika kufikia maendeleo bora. Ni muhimu kushikilia umoja wa kweli, kuunda ubia wa maendeleo wa kimataifa, na kuunda mazingira salama na thabiti ya kimataifa kwa maendeleo ya pamoja." alisema Xi.
Saudi Arabia yajipigia upato
Wakati tangazo hilo likionesha kuwa nchi zote sita zitajiunga, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan ameiambia televisheni ya Al-Arabiya kwamba Riyadh "inasubiri maelezo" kuhusu mwaliko huo na "itachukua uamuzi unaofaa", huku akisema nchi yake itakuwa na mchango mkubwa kwenye BRICS kutokana na fursa ilizonazo.
"Saudi Arabia ina uwezo unaofanya uchumi wake kuwa wa matumaini katika suala la kimaeneo, ina jiografia inayounganisha mabara matatu, na njia za maji zinazopakana nayo zinazoruhusu kufanya biashara ya kimataifa, pamoja na utajiri wake wa maliasili kwa nishati, madini, miradi ya nishati mbadala na miundombinu.” Alisema Mwanamfalme Faisal bin Farhan.
Kwa upande wake, Iran - ambayo kwa siku za karibuni imeimarisha uhusiano wake na hasimu wake Saudia kupitia upatanishi wa China, imesema inaunga mkono juhudi za BRICS za kuachana na muundo wa kibiashara unaotumia sarafu ya dola ya Marekani.
Soma pia: Ni kwa nini Saudia na nchi nyingine zataka uanachama BRICS?
Takriban nchi kumi na mbili zilikuwa zimetuma maombi rasmi ya kujiunga idadi kubwa miongoni mwao wakiwa kutoka kwa mataifa yasiyounga mkono Magharibi.
Fedha za kufadhili miradi
Huku haya yakijiri, Rais wa Benki ya New Development iliyoanzishwa na kundi hilo la BRICS, Dilma Rousseff, amesema benki hiyo inaweza kufadhili miradi itakayochangia katika kukabiliana na changamoto za dharura zaidi barani Afrika.
Rais huyo wa zamani wa Brazil amesema mataifa ya BRICS ni washirika wazuri kwa Afrika na kuongeza kuwa benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 itafadhili miradi ya miundombinu ya kawaida, ya kidijitali pamoja na ile ya elimu.
Soma pia: Putin hatahudhuria mkutano wa kilele wa BRICS nchini Afrika Kusini
BRICS ilianzishwa mwaka wa 2009 na kupanuliwa mwaka uliofuata kwa kujumuisha Afrika Kusini. China imekuwa ikifanya kampeni ya kulikuza kwa haraka kundi hilo ili kuwa mshindani wa kundi la nchi saba tajiri la G7 huku kukiwa na ushindani wa kimkakati na Marekani.
Vyanzo AFP/ Reuters