Vyombo vya usalama vya Tanzania vyalaumiwa kwa mauaji
10 Septemba 2024Taasisi ya Mwalimu Nyerere inatoa tamko hili siku moja baada ya aliyekuwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Chadema Ali Kibao kuzikwa jana Jumatatu mkoani Tanga baada ya kutekwa na kisha kuuawawa jijini Dar es salaam.
Butiku amesema vitendo vya utekaji, unyanyasaji na mauaji siyo hulka ya Tanzania.
Butiku ambaye alikuwa akuzungumza na waandishi wa habari amesisitiza kuwa taifa la Tanznaia siyo taifa la wahuni wala wauaji bali ni taifa linaloendeshwa kwa kufuata misingi ya katiba na sheria zake.
Amesema ni muhimu Rais Samia akapewa taarifa sahihi na vyombo vya ulinzi na usalama na kuongeza kuwa licha ya kwamba suala la ulinzi na amani ya nchi ni jukumu la kila raia, lakini vyombo vyenye dhamana katika eneo hilo vinapaswa kuwajibika.
Amesema vyombo hivyo vinajua yale yanayoendelea hivyo haviwezi kukwapa lawama na vinapaswa kuwajibika.
Tangu kuzuka upya kwa wimbi la utekaji na unyanyasaji vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa katikati ya kidole cha lawama huku chama kikuu cha upinzani kimekuwa kikililaumu jeshi la polisi.
Mauaji ya kiongozi huyo wa Chadema yamelaniwa vikali na viongozi wa kisiasa, taasisi za kiraia pamoja na jumuiya ya kimataifa.
Ubalozi wa Marekani umehimiza kuwepo kwa uchunguzi wa kina ikisema vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika uwanda wa demokrasia. Ubalozi wa Canada umeikaribisha hatua ya Rais Samia kuhimiza uchunguzi wa haraka juu ya tukio hilo.
Chadema imepanga kukutana wakati wowote kuanzia sasa kufuatia mauji ya kiongozi wake huyo kabla ya kutoa msimamo wake kwa umma. Viongozi wake wengine watatu wanaodaiwa kutekwa katika siku za hivi karibuni hawajulika waliko hadi sasa.
Kumekuwa na hali ya wasiwasi miongoni mwa jamii kutokana na kuongezeka kwa wimbi la watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Hivi karibuni chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society kilitoa orodha ya watu 87 iliyodai wametekwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.