1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibao azikwa, Masauni ashinikizwa kujiuzulu

9 Septemba 2024

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amejikuta katika wakati mgumu baada ya waombolezaji kwenye msiba wa kada wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA Ali Mohamed Kibao, kumtaka ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/4kQfD
Tanzania | Viongozi wa CHADEMA wakiwa wamebeba jeneza la Kibao
Mwili wa marehemu Ali Mohamed Kibao ukiwa umebebwa tayari kwa mazishi yaliyofanyika mkoani TangaPicha: Ericky Boniface /DW

Ingawa wanasiasa na wadau wa siasa, wanakubaliana na sauti za wananchi hawa, wanasema ingawa kujiuzulu hakuwezi kuwa suluhu, lakini ni hatua.

Hayo yanajiri siku moja tu baada ya kada wa CHADEMA na Mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, Ali Mohamed Kibao, kukutwa amefariki eneo la Ununio jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni aliyehudhuria swala ya mazishi ya Kibao Jumatatu hii, alijikuta katika wakati mgumu baada ya waombolezaji kugeuka mbogo, mara tu baada ya kunyanyuka ili kutoa dua  kwa niaba ya serikali, wakimtaka kiongozi huyo kujiuzulu.

Viongozi wa CHADEMA walioshiriki mazishi hayo, walitoa salamu zao za rambirambi na kumshinikiza waziri huyo mwenye dhamana ya ulinzi na usalama kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia usalama wa raia.

Tanzania | Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni na Freeman Mbowe
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania Hamad Masauni (katikati) akizungumza na kiongozi wa wa CHADEMA Freeman Mbowe (kulia) kwenye mazishi ya KibaoPicha: Ericky Boniface /DW

Kiongozi mkuu wa Chama cha Upinzani cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema inawezekana kujiuzulu kukawa sio suluhisho, lakini ni hatua.

Kibao alikutwa amekufa baada ya kutekwa

Kada huyo wa CHADEMA, alitekwa Septemba 6, akiwa katika basi la abiria la Tashrif, lililokuwa likielekea mkoani Tanga kutokea Dar es Salaam, na mwili wake kupatikana Septemba 8, katikaa eneo la Tegeta Ununio, jijini Dar es Salaam.

Jana, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi kupitia ukurasa wake wa X kufuatia kifo hicho na kuzitaka mamlaka kufanya uchunguzi na kumpa ripoti.

Jumuiya ya Kikristo Tanzania, CCT, kupitia Mwenyekiti wake Askofu Frederick Shoo, imekemea vikali mauaji hayo na kuiwataka Watanzania waombe na kukemea vitendo hivyo.

Huu ni mfululizo wa matukio ya watu kutekwa na wengine kukutwa wakiwa wamefariki. Mwezi Juni mwaka huu Edgar Mwakabela maarufu Sativa, mkazi wa Dar es Salaam alitoweka nyumbani kwake, na baadaye alipatikana akiwa amejeruhiwa huko mkoani Katavi.

Soma zaidi: Mwanasiasa wa upinzani 'alietekwa' Tanzania akutwa amekufa