Kampeni za mwisho mwisho Afrika Kusini kabla ya uchaguzi
26 Mei 2024
Uchaguzi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko muhimu nchini Afrika Kusini baada ya miongo mitatu.
Maelfu ya wafuasi wa chama kinachotawala cha African National Congress, ANC waliovalia nguo za rangi ya chama chao ambayo ni nyeusi, kijani na manjano walikusanyika katika uwanja wa soka mjini Johannesburg siku ya Jumamosi, kusikiliza hotuba ya kiongozi wa chama chao cha ANC ambaye pia ni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Soma Zaidi: Afrika Kusini: ANC yatuhumiwa kutaka kumuua rais Zuma
Ramaphosa katika hotuba yake alikiri kwamba anayatambua malalamiko ya raia wa Afrika Kusini, ambayo ni pamoja na umaskini uliokithiri na ukosefu wa ajira, maswala ambayo yanawaathiri zaidi wananchi Weusi walio wengi nchini humo.
Ahadi ya Ramaphosa
Rais Ramaphosa amewaahidi Waafrika Kusini kwamba chama chake iwapo kitarudishwa madarakani kitayashughulikia maswala hayo ya ajira, ustawi wa jamii na kero nyingine zinazowakabili wananchi.
Chama cha ANC kinakabiliwa na shinikizo kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa la kwamba huenda kikapoteza idadi kubwa ya wabunge ambao walikifanya chama hicho kuwa na wingi wa viti bungeni wakati wote wa miaka 30 kilipokuwa madarakani tangu kumalizika kwa utawala wa Weupe wachache mnamo mwaka 1994.
Soma Zaidi:Ramaphosa anusurika kura ya kumuondoa madarakani
Iwapo utabiri wa kura za maoni utathibitika kuwa sahihi, chama cha ANC, ambacho kinakabiliwa na kashfa za ufisadi, ukosefu wa ajira na hali mbaya ya uchumi kinaweza kupata chini ya asilimia 50 ya kura. Na hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho tangu kilipoingia madarakani chini ya uongozi wa shujaa wa ukombozi Nelson Mandela.
Chama Kikuu cha upinzani cha DA
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kilifanya mkutano wake mjini Cape Town, jiji la pili kwa ukubwa nchini Afrika Kusini na ambao ni ngome kuu ya chama hicho.
Kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen, alitoa hotuba mbele ya wafuasi wa chama hicho cha DA wakiwa wamevalia mavazi ya chama chao ambayo ni rangi ya buluu huku wakiwa wamebeba miavuli ya buluu pia.
Soma Zaidi:Uchaguzi wa Afrika Kusini mtihani kwa Ramaphosa
Steenhuisen aliwauliza wafuasi wa chama hicho kwa kusema: "Wanademokrasia, marafiki, je mko tayari kwa mabadiliko?" na umati wa watu ulijibu kwa kelele "Ndiyo!"
EFF yasema iko tayari kuiongoza Afrika Kusini
Chama cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi cha mrengo wa kushoto cha EFF, kinachoongozwa na Julius Malema kilifanya kampeni yake ya mwishoni mwa wiki katika mji wa kaskazini wa Polokwane, mji wa uzawa wa kiongozi wa chama cha EFF Julius Malema.
Malema aliwaambia wafuasi wake kwamba Watu wa Afrika Kusini lazima waamue kama wanaupendelea ukosefu wa ajira au la."
Amesema EFF iko tayari kupambana na kila aina ya uhalifu ndani ya nchi, ikiwa ni pamoja na ufisadi wa wanasiasa.Julius Malema, mwenye umri wa miaka 43, alikuwa zamani kiongozi wa tawi la vijana la ANC.
Kampeni ya chama Zuma cha MK
Chama kipya cha MK cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma pia kilifanya kampeni yake katika kitongoji kilicho nje kidogo katika mji wa pwani ya mashariki wa Durban, ingawa Zuma hakuhudhuria hafla hiyo lakini binti yake Duduzile Zuma-Sambudla, alihudhuria mkutato huo.
Zuma mwenye umri wa miaka 82 alitikisa siasa za Afrika Kusini alipotangaza mwaka jana kwamba a^nakipa kisogo chama chake cha zamani cha ANC na kujiunga na chama cha MK, huku akiikosoa vikali ANC chini ya uongozi wa Cyril Ramaphosa.
Soma Zaidi: Zuma hapaswi kushiriki uchaguzi wa bunge
Zuma amezuiwa kuwania nafasi yoyote katika uchaguzi kwa sababu ya hatia ya jinai ya hapo awali, lakini chama chake cha MK kinaruhusiwa kutumia sura yake kama kiongozi wake na yeye amekuwa akiendelea kukifanyia kampeni chama chake.
Uchaguzi wa Afrika Kusini hufanyika vipi?
Waafrika Kusini kwa mujibu wa sheria ya nchini mwao huvipigia kura vyama na sio rais katika uchaguzi huo wa mkuu. Na vyama vya siasa vinapopata viti vingi Bungeni ndio vinakuwa na uwezo mkubwa kumchagua rais kupitia kwa wabunge wake.
Ndio kusema iwapo chama cha ANC kitapoteza wingi wa wabunge wake basi hatua hiyo itamwathiri Cyril Ramaphosa mwenye umri wa wa miaka 71 ambaye matumaini yake ni kuchaguliwa tena ili ahudumu muhula wa pili wa miaka mitano na wa mwisho.
Soma Zaidi: Chama cha ANC chafungua kampeni za uchaguzi chini ya shinikizo
Hata hivyo baadhi ya wafuasi wa chama cha ANC wameonyesha kutorodhika na chama chao kutokana na nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 62 bado wanapambana na umaskini, ukosefu mkubwa wa ajira, matatizo ya ufisadi, uhalifu na serikali kushindwa kutoa huduma za msingi kwenye baadhi ya maeneo.
Vyanzo:AP/RTRE