1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Julius Malema aondolewa kwa miaka mitano

10 Novemba 2011

Chama tawala cha African National Congress ANC cha Afrika Kusini kimemkuta na hatia kiongozi wake mwenye utata na ushawishi mkubwa Julius Malema kwa kuvuruga mikutano ya chama hicho.

https://p.dw.com/p/138Dj
Kiongozi wa ANC tawi la Vijana Julius MalemaPicha: AP

Kulingana na maafisa katika kamati ya nidhamu ya chama tawala cha ANC nchini Afrika kusini, hatua ya Julius Malema kiongozi wa chama hicho tawi la vijana  kwenda katika mikutano ya ANC bila kualikwa na kuzusha vurugu katika mikutano hiyo ni jambo lililosababisha kamati ya nidhamu kutoa hukumu hiyo. Maafisa hao wamesema Malema amekuwa akikiuka sheria za chama hicho mara kwa mara.

Habari zaidi zinasema sasa Malema amesimamishwa kama kiongozi wa chama cha ANC kwa muda wa miaka mitano. Kutokana na uamuzi huu hatma ya kisiasa ya Malema aliye na umri wa miaka 30 na ambaye pia ana ushawishi mkubwa nchini Afrika Kusini inaonekana kumalizika.

ANC-Kongress in Durban
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: picture alliance / dpa

Baadhi ya wanachama wa ANC wanasema Malema alikuwa mbioni kumtoa Zuma kama rais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa disemba mwaka ujao kufuatia umaarufu wake mkubwa ambao kwa sasa milioni ya raia afrika kusini wanamuona tayari kama kiongozi.

Hata hivo polisi mjini Johannesburg wamezunguka mjini humo hasaa katika makao makuu ya chama cha ANC ili kuzuia marudio ya ghasia yaliofanyika mwezi wa Agosti ambapo wafuasi wa Julius Malema walizua vurugu kali wakati kesi hiii ilipokuwa inaanza.

Luteni Lungelo Dlamini mkuu wa polisi mjini humo amesema kwa sasa bado hakujatokea ghasia zozote lakini polisi wako tayari kuzima vurugu la aina yeyote itakayotokea.

Malema pamoja na wenzake watano walishtakiwa kwa kuchochea mgawanyiko na kuvunja heshima ya chama cha ANC. Kulingana na wanaharakati wa kisiasa nchini humo sasa wanasema hatua hii ya malema kupatikana na hatia na kusimamishwa kwa miaka mitano inaweza kumpa nafasi rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma nafasi ya pili ya utawala nchini humo katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mwaka ujao.     

Hukumu hii hata hivyo imeleta hofu kubwa  miongoni mwa raia nchini humo ambao wengi wanasema sasa kuna wasiwasi wa kutokea kwa vurugu kufuatia Malema kuwa na wafuasi wengi nchini humo ambao bila shaka hawatakubali hukumu hiyo.

Mwandishi Amina Abubakar/RTRE/AFPE

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman