1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen: Siku zijazo Ulaya huenda zikawa ngumu

14 Septemba 2022

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya ametahadharisha leo juu ya nyakati ngumu zinazozikabili kaya na biashara barani Ulaya kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na vita vya nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4GosU
Frankreich | Ursula von der Leyen im Straßburger Europaparlament
Picha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Akilihutubia bunge la Ulaya mjini Strasbourg nchini Ufaransa, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amekiri kuwa siku zijazo barani Ulaya hazitakuwa rahisi, sio tu kwa familia zinazopitia changamoto za kifedha bali pia wasiwasi wa kuyumba kwa biashara.

Soma pia: Marekani kutoa msaada wa dola bilioni 2 kwa Ukraine

Von der Leyen ameongeza kuwa sio Ukraine tu inayopitia msukosuko bali Ulaya na dunia nzima inakodolea macho hali ya wasiwasi.

Amesema, "Niwe muwazi kabisa. Hivi sio vita vilivyoanzishwa na Urusi dhidi ya Ukraine bali ni vita dhidi ya nishati yetu, uchumi wetu na maadili yetu. Ni vita dhidi ya mustakabali wetu." 

Ametangaza pendekezo la kisheria la kulazimisha ushuru wa mapato kwa makampuni ya nishati. Ushuru huo wa ziada ambao unaweza kufikia zaidi ya euro bilioni 139.6, unatarajiwa kuzisaidia kaya na biashara za Umoja huo zinazoyumbayumba.

Von der Leyen ameweka bayana kuwa katika nyakati hizi ngumu, faida lazima igawanywe na kulekezwa kwa wenye mahitaji zaidi.

"Mwaka jana, gesi ya Urusi ilichangia asilimia 40 ya gesi yetu iliyoagizwa kutoka nje. Leo kiwango hicho kimeshuka hadi asilimia tisa. Lakini pia tunaona kwamba Urusi inaendelea kudhibiti soko letu la nishati. Urusi inajaribu kuongeza bei ya nishati kinyume kabisa na mikataba iliyoko. Soko hili la nishati halifanyi kazi tena," amesema von der Leyen.

Mfumuko wa bei umeongeza wasiwasi wa kudorora kwa uchumi Ulaya

Protest gegen steigende Energiepreise und steigende Lebenshaltungskosten in Leipzig
Raia wa Ujerumani wakiandamana mjini Leipzig wakilalamikia juu ya kupanda kwa gharama ya maishaPicha: Christian Mang/REUTERS

Mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 9.1 katika mataifa yanayotumia sarafu ya Euro kufikia mwezi Agosti, kwa kiasi kikubwa ulichochewa na gharama ya nishati iliyopanda hadi asilimia 38.3 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Mfumuko huo wa bei umeongeza wasiwasi wa uwezekano wa kudorora kwa uchumi katika mataifa ya Ulaya.

Aidha rais huyo wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amesema mfululizo wa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vitaendelea kuwepo na kwamba mataifa ya Umoja huo yanafaa kusalia imara dhidi ya vitisho vya Urusi.

Soma pia: UN: Urusi inawachukua kwa nguvu watoto wa Ukraine

Mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska aliyehudhuria mkutano huo mjini Strasbourg, alishangiliwa na wabunge kutokana na kuonyesha ujasiri dhidi ya ukatili wa Putin.

von der Leyen aliyekuwa amevaa nguo zenye rangi ya samawati na njano, iliyoko kwenye bendera ya Ukraine kama ishara ya kuiunga mkono nchini hiyo, amewaambia wabunge katika bunge hilo la Ulaya kuwa atasafiri hadi Kiev kufanya mkutano na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili kwa undani zaidi kile kilichoelezwa kuwa muendelezo wa msaada wa Ulaya kwa taifa hilo la Ulaya mashariki.