Marekani kutoa msaada wa dola bilioni 2 kwa Ukraine
8 Septemba 2022Tangazo hilo limetolewa Alhamisi wakati wa ziara ambayo haikutangazwa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken mjini Kiev katika juhudi za kuiunga mkono Ukraine kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi.
Msaada na nchi jirani pia
Msada huo wa ziada wa muda mrefu wa kijeshi kwa Ukraine utazihusu pia nchi jirani 18 zikiwemo wanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na washirika wa usalama wa kikanda ambazo ziko katika hatari ya kuvamiwa na Urusi katika siku zijazo.
Blinken, ambaye hii ni ziara yake ya pili mjini Kiev tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, amekutana na Waziri mwenzake, Dmytro Kuleba Pamoja na wanadiplomasia wa Marekani na pia ameitembelea hospitali ya Watoto ambako alikutana na vijana waliojeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi.
Msaada huo mpya umetolewa muda mfupi baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin kuahidi msaada mwingine wa kijeshi wa dola milioni 675 kwa Ukraine.
Akizingumza katika mkutano wa washirika wa Marekani katika kambi ya jeshi la anga nchini Ujerumani ya Ramstein, Austin amesema msaada huo utahusisha maroketi aina ya GMLRS, mizinga inayojifyatua yenyewe aina ya Howitzer, silaha za kivita, magari ya kivita ya kubebea wagonjwa, mifumo ya kujikinga na makombora na silaha ndogo ndogo.
Vikosi vya Urusi vyaendeleza mashambulizi Ukraine
"Vikosi vya Urusi vinaendelea kuishambulia miji ya Ukraine na raia kwa makombora na mizinga. Lakini vikosi vya Ukraine vimeanza operesheni yao ya kulikomboa eneo la kusini mwa nchi yao. Na wanajumuisha uwezo ambao wote tumechangia ili waweze kujisaidia kupigana na kulirejesha eneo lao huru," alifafanua Austin.
Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin amesema Alhamisi kuwa vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya Urusi vimeshindwa kuidhoofisha uthabiti wa kifedha wa Urusi.
Matamshi hayo ameyatoa leo katika Jukwaa la Kiuchumi linalofanyika mjini Moscow. Anasema walitabiriwa kuwa na mdodoro mkubwa wa kiuchumi, lakini hilo halijatokea na kwamba Urusi itaibuka imara na hata kuwa na nguvu zaidi.
Na katika uwanja wa mapambano, wanahabari wanaoripoti vita vya wa Urusi wamesema jeshi la Ukraine limefanikiwa kusonga mbele karibu na mji wa Balakliya, na kuvikomboa vijiji kadhaa tangu mwanzoni mwa wiki hii.
Ukraine: Urusi inataka kukihujumu kinu cha Zaporizhzhia
Ama kwa upande mwingine, Petro Kotin mkuu wa shirika la nishati nchini Ukraine, Energoatom Alhamisi ameishutumu Urusi kwa kujaribu kukiiba kinu kikubwa kabisa cha nishati ya nyuklia barani Ulaya cha Zaporizhzhia kwa kukitenganisha na gridi ya umeme ya Ukraine na kukiacha kikiwa hatarini kukumbwa na janga la mionzi.
Wakati huo huo, Poland itaungana na mataifa ya eneo la Baltic katika kuwazuia raia wa urusi kuingia kwenye nchi zao kuanzia Septemba 19.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Alhamisi, mawaziri wakuu wa Estonia, Latvia, Lithuania na Poland wamesema haikubaliki kwamba raia wa serikali chokozi wanaweza kusafiri kwa uhuru katika nchi za Umoja wa Ulaya, wakati huo huo, watu wa Ukraine wanateswa na kuuawa.
(AFP, AP, Reuters)