Vita Ukraine: Uchumi wa Urusi wasalia imara licha ya vikwazo
23 Februari 2024Mataifa ya Ulaya na Marekani yalikisia kwamba vikwazo vingi dhidi ya taifa hilo kutoka jamii ya kimataifa kufuatia uvamizi huo wa Februari 2022, vingezorotesha kabisa uchumi wa taifa hilo.
Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF hivi karibuni lilisema kwamba Pato la Ndani la Taifa, GDP linaweza kuongezeka kwa asilimia 2.6 nchini Urusi kwa mwaka huu, likiwa ni ongezeko kutoka makadirio yake ya mwezi Oktoba.
Wakati huohuo, mapato ya mafuta kwa mara nyingine yanaongezeka na kiwango cha ukosefu wa ajira nacho kimeshuka katika namna ambayo haijashuhudiwa kwa muda mrefu.
Soma pia: Vita vya Urusi nchini Ukraine vyakaribia mwaka wa tatu
Ikulu ya Kremlin imeongeza kwa kiasi kikubwa sana matumizi ya ulinzi. Asilimia 40 ya bajeti yake ya mwaka 2024 itakuwa ni ya masuala ya ulinzi na usalama. Huo ni uchumi wa kivita, wanasema wachambuzi, wakati kukiwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi na mfumuko mkubwa wa bei. Vikwazo pia vimeendelea kuleta athari.
Ni kwa namna gani Urusi ilifanikiwa na kuvishinda vizuizi vya magharibi?
Elina Ribakova, mchumi anayefanya kazi na Taasisi ya masuala ya uchumi ya Peterson, ameiambia DW kwamba kuna sababu tatu kubwa zinazoelezea hali hii, akimaanisha uchumi wa Urusi kuendelea kuimarika licha ya changamoto zote.
Kwanza ni kwamba mfumo wa kifedha wa Urusi ulioandaliwa vya kutosha kukabiliana na wimbi la vikwazo vya kibenki na kifedha tangu wakati ilipokabiliwa na hatua kali baada ya kuinyakua Rasi ya Crimea mnamo 2014.
Pili ilikuwa ni kwamba mwaka 2022, Urusi ilikuwa inajipatia mapato makubwa ya biashara ya mafuta na gesi kwa kuwa mataifa ya magharibi hayakuweza kulenga biashara za nje na hata katika wakati ambapo bei zilipanda baada ya uvamizi nchini Ukraine.
Na tatu ni udhibiti duni wa mauzo ya nje ambao haujaweza kuizuia Urusi kutumia nchi ya tatu kupata bidhaa inayoihitaji kwa ajili ya viwanda vyake vya kijeshi.
Soma pia: Vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa Urusi vinatekelezwa?
Hata hivyo, Benjamin Hilgenstock kutokea Shule ya Uchumi ya mjini Kyiv anasema ni muhimu kukumbuka kwamba wakati uchumi wa Urusi ukiwa katika hali nzuri kuliko ilivyotarajiwa, vikwazo bado vina athari kubwa, akiangazia kwa mfano kushuka kwa mapato ya mauzo ya nje ya bidhaa za mafuta na gesi kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Ameangazia pia agizo lililotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden mwezi Disemba lililoidhinisha vikwazo vinavyowezekana dhidi ya benki za kigeni zinazoruhusu miamala inayosaidia kufadhili kambi za kijeshi na viwanda ya Urusi.
Mashaka ya uchumi wa kivita
Kichocheo kingine muhimu kwenye uchumi wa Urusi ni matumizi makubwa ya kiulinzi, ambayo yameongezeka mara tatu tangu 2021. Ribakova anasema Urusi kwa sasa ina uchumi wa vita ambao anaamini unakuza Pato la Taifa.
Soma pia: Je Ulaya yahitaji kutangaza "uchumi wa wakati wa vita"?
Lakini Chris Weafer, mshauri wa uwekezaji aliyefanya kazi nchini Urusi kwa zaidi ya miaka 25, anasema kutakuwa na matokeo mabaya na ya muda mrefu ikiwa matumizi ya ziada yatajikita kwenye bidhaa "zinazotumika" badala ya uwekezaji kwenye viwanda.
Anasema jambo jingine ni kwamba uchumi wa vita huathiri soko la ajira na hasa kwa kuwa karibu wafanyakazi milioni 1 wenye ujuzi wa juu wameondoka Urusi tangu 2022, hii ikimaanisha sasa kuna uhaba wa wafanyakazi.
Je Utadumu?
Kulingana na Weafer, msingi mkubwa wa rasilimali nchini humo umepuuzwa mara kwa mara wakati vikwazo vilipowekwa, akiangazia umuhimu ulioendelea kuwekwa kwenye mafuta na gesi yake katika masoko ya kimataifa na bidhaa nyingine kama za uranium, ambazo Marekani bado inanunua kwa wingi.
Kulingana naye, Urusi inadhani uchumi wake uliimarika kwa mwaka 2022 ama 2023, lakini sasa utazorota kutokana na matumizi makubwa ya kijeshi.
Kwa Ribakova, hatma ya Ukraine inabakia kushikamana kwa karibu na hali ya uchumi wa Urusi. Anasema, kwa kuwa vikwazo havikutosha kuukomesha uvamizi wa Urusi, ni muhimu kwa muungano wa Magharibi kuchukua hatua zaidi ili kupunguza uwezo wa Kremlin.