1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wapya wa Kenya watakiwa kuheshimu haki za binaadamu

25 Aprili 2013

Shirika la kutetea haki za binaadamu ulimwenguni la Human Rights Watch,limewataka viongozi wapya wa Kenya kufanya mabadiliko katika mambo manne makuu ambayo yanachangia kuvunja haki za binadamu kwa kiasi kikubwa.

https://p.dw.com/p/18Mrc
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: Reuters

Wito huo wa Human Rights Watch umetolewa katika ripoti yake ya kurasa 11 ukiwataka viongozi wa Kenya kukomesha vitendo vya uvunjaji wa haki za binaadamu,kuheshimu uhuru wa kuongea, kulinda na kutetea haki za binaadamu,kufanya mabadiliko katika umiliki wa ardhi na kushirikiana moja kwa moja na mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa kivita, ICC, iliyopo mjini The Hague, nchini Uholanzi.

Wadau wa habari
Wadau wa habariPicha: DW

Mkurugenzi wa Shirika hilo, Afrika Daniel Bekele, amesema kuwa ili kutimiza ahadi walizotoa viongozi wapya wa Kenya kwa vitendo, itahitaji kuangalia makosa yaliyopita na ya sasa ya uvunjaji wa haki za binaadamu na haki kuchua nafasi yake katika mahakama za ndani na ICC.

Uchunguzi uliofanywa na Human Rights Watch, umebaini kuwa kuna mashtaka dhidi ya watu watatu ambao serikali ya Kenya bado haijawashtaki, maafisa wa polisi na baadhi ya watu waliopanga machafuko ya mwaka 2007-2008.

Mwaka jana mwendesha mashtaka mkuu wa Kenya alidai kuwa ofisi yake ilipitia kesi 5,000 za machafuko ya mwaka 2007-2008, na kusema kuwa ofisi hiyo ilishindwa kupata ushahidi wa kutosha wa kuendelea na mashtaka hayo.

Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta, na Makamo wake William Ruto wanakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya ICC ya mjini The Hague, kwa kuchangia katika ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007.

Vyombo vya habari mjini Nairobi Kenya
Vyombo vya habari mjini Nairobi KenyaPicha: DW/M.Meier

Wawili hao waliapishwa April 9 mwaka huu baada ya mahakama kuu nchini humo kuthibitisha ushindi wao, ambapo Kenya kama nchi iliyotia saini mkataba wa Roma ulioiunda mahakama ya ICC ina wajibu wa kutoa ushirikiano mzuri na mahakama hiyo.

Mbali na hilo serikali ya Kenya imetakiwa kuwalinda watetezi wa haki za binaadamu nchini humo, vyombo vya habari, na kuwachukulia hatua kali waliohusika katika kuwatesa wanaharakati wa haki za binaadamu na waandishi wa habari, na wakosoaji wa kawaida.

Lazima kuheshimu haki za binaadamu

'Ili kuhakikisha ushirikiano kati ya Kenya na mahakama ya ICC unapatikana, vyombo vya sheria nchini Kenya vinatakiwa kufanyia kazi mashtaka yaliyopita, na kuandaa miundombinu maalumu ya uchunguzi wa mashtaka mapya ili kuondoa utabaka katika uajibishaji'' amesema Bekele mkurugenzi wa Human Rights watch.

Miezi ya hivi karibuni waandishi wa habari 19 wametishiwa na watu wasiojulikana katika eneo la Eldoret nchini Kenya na kufanya mateso na mashambulizi dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu ambayo yanaonekana kupangwa na watu wanaotuhumiwa na ICC.

Hivi karibuni waandishi wa habari wawili na watetezi wa haki za binaadamu wanne wameuawa na wengine kutishiwa mwishoni mwa mwaka 2012 na mwaka huu wa 2013, kufuatia uchunguzi ambao unadaiwa kufanywa na mahakama.

Machi 30 mwaka huu mwandishi wa habari wa gazeti huru la The star, Bernard Wesonga, alikutwa amekufa nyumbani kwake, katika mji wa bandari wa Mombasa, baada ya kupokea vitisho kupitia simu yake ya mkononi, kuhusu habari anazoandika.

Mbali na huyo, mwandishi wa Televisheni ya KTN Kenya akiongea na Human Rights Watch amedai anapokea ujumbe wa vitisho, hasa baada ya kurusha ripoti ya uchunguzi April 7, 2013, iliyoonesha kuwa aliyekuwa makamo wa Rais na waziri wa usalama wa ndani, hayati Profesa George Saitoti, aliyefariki katika ajali ya helikopta mwaka 2012, ni muhanga wa magenge ya vigogo wanaouza dawa za kulevya.

Februari mwaka huu, msemaji wa serikali ya Kenya, Muthai Kariuki, alimuonya mwandishi wa habari wa nje akisema kuwa ''tutakuchoma moto kabla ya kutuchoma sisi''na baada ya uchaguzi wa Machi 4 mwaka huu wizara ya habari na mawasiliano ya umma ilitishia kuwarudisha waandishi wa nje.

Kufuatia hali hiyo Bekele amewataka viongozi wa Kenya kulinda haki ya kikatiba ya uhuru wa kuongea, kufanya mikutano na kuondoa hali ya wasiwasi, kufanya uchunguzi na kuwashitaki waliohusika katika mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na wanahakati wa haki za binaadamu kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi.

Mwandishi:Hashim Gulana

Mwandishi:Josephat Charo