Viongozi wataka uwekezaji zaidi katika Nishati Jadidifu
25 Septemba 2024Viongozi wa dunia wametoa wito wa uwekezaji zaidi katika nishatijadidifu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku mataifa yanayoendelea yakisema yanahitaji msaada wa kifedha kufanya mabadiliko hayo.
Akizungumza katika Mkutano wa kilele wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu, unaofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais wa Kenya William Ruto, alitoa hoja ya kuwekeza kwenye nishati hiyo safi barani Afrika kama sehemu ya ahadi ya kimataifa iliyotolewa katika mkutano wa kilele wa COP28 wa mwaka jana ya kuongeza uwezo wa nishati safi mara tatu ifikapo 2030.
Ruto aliuambia mkutano huo kwamba Afrika inapokea chini ya 50% ya uwekezaji wa kimataifa wa nishati jadidifu licha ya kuwa eneo lenye 60% ya fursa bora zaidi duniani ya nishati inayotokana na jua.
Rais huyo ameongeza kuwa Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali zinazohitajika kwa maendeleo, lakini mara nyingi haiwezi kufikia rasilimali hizo kutokana na mchanganyiko wa sasa wa nishati isiyoweza kutegemewa au ya gharama kubwa.
Soma: Viongozi wa Afrika wahimiza matumizi ya nishati jadidifu
Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley alisema kuwa ruzuku ya mafuta ya visukuku inaizidi ruzuku ya nishati mbadala, ambayo inafanya ughali zaidi kwa mataifa madogo kuendeleza miradi ya nishati safi.
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliuambia mkutano huo kwamba hilo litahitaji "uwekezaji mkubwa" kutoka kwa sekta ya umma na ya kibinafsi, haswa kwa "nchi na maeneo ambayo kuna ukosefu wa nishati na mitaji ya bei nafuu, na ambapo gharama ni kubwa sana na kikwazo katika usambazaji wa umeme."
Soma: Guterres aurai ulimwengu kuisaidia Afrika kuwa mzalishaji mkubwa wa nishati jadidifu
Azerbaijan, ambayo itakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwaka huu wa mazingira COP29 mwezi Novemba, ilisema inapanga kuhamasisha serikali kutoa ahadi mpya za kimataifa ili kuongeza hifadhi ya umeme mara sita.
Muungano wa baadhi ya makampuni makubwa duniani, taasisi za kifedha zimeitaka serikali kupitisha sera ambazo walisema zinaweza kukusanya kiasi cha hadi dola trilioni 1 katika uwekezaji wa nishati safi ifikapo 2030.
Baadhi ya kampuni na wawekezaji wanaitizama teknolojia ya Akili Mnemba kwa shauku kubwa kwa ajili ya upatikanaji wa suluhisho katika sekta ya nishati.
Viongozi wa Afrika wanajaribu kutafuta njia za kukuza sekta ya nishati, ili kuchochea maendeleo na kufikia mahitaji ya mamilioni ya watu ambao bado hawana umeme hata kidogo.Azimio la Nairobi la hali ya hewa kutiwa saini
Benki ya Maendeleo ya Afrika na marais wa Benki ya Dunia walizungumza Jumatatu kuhusu mradi wao wa kupanua upatikanaji wa umeme kwa zaidi ya watu milioni 300 katika bara hilo, ambapo benki hizo zilikuwa zikitafuta dola bilioni 30 katika uwekezaji wa sekta binafsi.