Viongozi wa dunia wahimiza uwekezaji katika nishati jadidifu
25 Septemba 2024Viongozi wa dunia jana walitoa wito wa uwekezaji zaidi katika nishati jadidifu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku mataifa yanayoendelea yakisema yanahitaji msaada wa kifedha kufanya mabadiliko hayo.
Akizungumza katika Mkutano wa kilele wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu, (Global Renewables Summit) unaofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa MataifaRais wa Kenya William Ruto, alitoa hoja ya kuwekeza kwenye nishati hiyo rafiki barani Afrika kama sehemu ya ahadi ya kimataifa iliyotolewa katika mkutano wa kilele wa COP28 wa mwaka jana ya kuongeza uwezo wa nishati safi mara tatu ifikapo 2030.
Ruto aliuambia mkutano huo kwamba Afrika inapokea chini ya 50% ya uwekezaji wa kimataifa wa nishati jadidifu licha ya kuwa eneo lenye 60% ya fursa bora zaidi duniani ya nishati inayotokana na jua.
Rais huyo ameongeza kuwa Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali zinazohitajika kwa maendeleo, lakini mara nyingi haiwezi kufikia rasilimali hizo kutokana na mchanganyiko wa sasa wa nishati isiyoweza kutegemewa au ya gharama kubwa.