Viongozi wa Ulaya wataka Umoja wa Ulaya uimarishwe
25 Januari 2018Akizungumza jana jioni katika Kongamano la Kiuchumi Duniani linalofanyika Davos, Uswisi, Rais wa Ufaransa Emannuel Macron, alielezea mtazamo makini kwa ajili ya Ulaya wakati akizungumzia kuhusu mkakati wa miaka 10 wa kuufanyia mageuzi makubwa Umoja wa Ulaya ili uweze kuwa na nguvu zaidi. Macron alisema Umoja wa Ulaya lazima uwe mchangiaji imara pindi yanapoibuka masuala muhimu ya kimataifa.
''Maoni yangu ni kwamba tunapaswa kuweka upya mkakati wa miaka 10, kwa sababu sio mkakati wa usiku mmoja. Mkakati wa miaka 10 ili kuifanya Ulaya kuwa halisi kiuchumi, kijamii, kisayansi, kimazingira na kisiasa. Hilo ndilo tunapaswa kulijenga, jambo linalomaanisha kwamba tunahitaji kuwa na uhuru zaidi na Ulaya iliyoungana na yenye demokrasia,'' alisema Macron.
Macron amesema alimshauri sana Trump kuhudhuria kongamano la Davos wakati walipozungumza kwa njia ya siku kuhusu Iran, kwa sababu aliona ni jambo jema kiongozi huyo wa Marekani kuelezea sera zake na dunia kwa ujumla katika mkutano huo.
Kwa upande wake, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema kujitenga sio suluhisho la matatizo ya kiuchumi duniani na suala hilo halitawasogeza mbele na kwamba wanapaswa kushirikiana. Aidha, ameutaka Umoja wa Ulaya kupitisha sera ya kigeni ambayo ni thabiti zaidi, huku akionya kwamba diplomasia ya umoja huo itadhoofika kama hawatoanza kupeleka ujumbe wa pamoja kwa nchi kama vile Marekani, China, India na Urusi.
Viongozi wengine wa Ulaya waliozungumza jana mjini Davos ni Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni na Mfalme wa Uhispania, Felipe wa Sita. Gentiloni alionya kuwa hamu ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuiweka ''Marekani Kwanza'' ni halali, lakini suala la kujitenga halina faida na kwamba wanachohitaji ni ukuaji wa uchumi na ustawi na kuwalinda wafanyakazi wao.
Trump awasili Davos
Hayo yanajiri wakati ambapo Trump amewasili leo mjini Davos kuhudhuria kongamano hilo la kiuchumi, huku akiwa na lengo la kuwashawishi viongozi wa kimataifa kuhusu ajenda yake ya ''Marekani Kwanza'', kwamba haina maana ya kujiondoa katika jukwaa la dunia. Trump anatarajiwa kuhutubia katika kongamano hilo kesho Ijumaa.
Kiongozi huyo wa Marekani anatarajiwa kuitumia ziara yake hiyo barani Ulaya kama fursa ya kufanya mazungumzo na washirika wake wa kisiasa. Trump amepangiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa Rwanda, Paul Kagame pamoja na mwenyeji wa kongamano hilo, Rais wa Uswisi, Alain Berset,.
Mazungumzo yao yanatarajiwa kuangazia masuala ya kichumi pamoja na uhusiano kati ya Marekani na mataifa hayo. Trump ambaye pia atakutana na viongozi wa kibiashara, ataitetea sera yake kuhusu mageuzi katika mfumo wa kodi nchini Marekani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga