Mizozo ya ulimwengu yagubika mkutano wa Munich
19 Februari 2024Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametoa wito wa kuwepo na mshikamano zaidi katika kuendeleza uwezo wa usalama na ulinzi barani Ulaya, wakati uwezekano wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kurejea madarakani ukizidisha wasiwasi miongoni mwa washirika wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami NATO.
Kivuli cha Trump kimeonekana kutawala kwa kiasi kikubwa siku ya kwanza ya mkutano wa 60 wa kimataifa wa usalama wa Munich, ambao hufanyika kila mwaka na kuwakusanya viongozi wa ulimwengu na wakuu wa ulinzi kujadili sera ya kimataifa ya usalama.
Ajenda kuu za mkutano huo wa siku tatu ni mizozo inayoendelea ya Ukanda wa Gaza na Ukraine.Urusi imejikuta katikati mwa ajenda kuu za mkutano huo, sio kwasababu tu ya uvamizi wake nchini Ukraine, lakini pia kutokana na taarifa za kifo cha kiongozi wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa Urusi Alexei Navalny, aliyeripotiwa kufa gerezani.
Akizungumza katika mkutano huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kwamba muungano wa Ulaya kwa miongo kadhaa umefurahia ushirikiano kiusalama wa Marekani. Aidha mwanadiplomasia huyo mkuu ameongeza kuwa inawezekana hakikisho hilo la usalama la Marekani lisiwe wazi wakati wote na kuutaka Umoja huo kuwa "huru zaidi" kuliko ilivyozoeleka.
Ulaya ilishikwa na khofu na kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Trump kwamba Urusi inapaswa kufanya chochote inachokitaka kwa wanachama wa NATO ambao wanashindwa kutimiza ahadi zake za kifedha katika jumuiya ya kujihami ya NATO.
Soma: Guterres kufunguwa Mkutano wa Usalama wa Munich
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kwa "kuzingatia hali ya ulimwengu, Ulaya inapaswa kuwekeza zaidi katika ulinzi", na kuongeza kuwa hivi karibuni, muungano huo utachapisha mkakati wa uwekezaji katika ulinzi.
Naye waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, amenukuliwa akisema kwamba ana shauku ya kukutana na wabunge wa Marekani katika mkutano huo, ili aweze kuwapa hakikisho kwamba Berlin "inafanya kazi yake" na inajitolea kubeba sehemu ya jukumu lake linapokuja suala la NATO.
Lakini kauli iliyotolewa na waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner inaashiria jinsi gani itakuwa vigumu kwa Ulaya kupata mwafaka wa pamoja kuhusu mkakati wa ulinzi. Lindner amesema kuwa anapinga Ujerumani kutumia fedha zaidi katika bajeti ya ulinzi kupita lengo la NATO la asilimia 2 ya pato la taifa.
Soma pia: Urusi, Iran hazikualikwa Mkutano wa Usalama wa Munich
Ameeleza kwamba "kwa kuzingatia kiwango cha uchumi wa Ujerumani, matumizi ya asilimia 2 katika ulinzi yanatosha". Waziri huyo amesisitiza nia yake ya kuona Ujerumani inaendeleza nidhamu ya kijadi katika matumizi ya fedha, akisema haja ya maboresho ya kijeshi hayamaanishi ndio iwe sababu ya kuitumbukiza Ulaya katika madeni.
Katika hotuba yake kwa hadhara ya mkutano huo, makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris alijaribu kuondoa wasiwasi kwamba Washington imekuwa mshirika asiyeaminika na msumbufu. Harris ametetea muungano wa NATO kama "kiini cha mtazamo wa usalama wa kimataifa" na kuapa Marekani itatimiza wajibu wake. Mkutano huo unaendelea leo ambapo viongozi kadhaa watatoa hotuba zao.