Viongozi wa Mediterania wakutana kujadili juu ya wahamiaji
29 Septemba 2023Mkutano huo unafanyika siku moja tu baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR kusema kwamba zaidi ya wahamiaji 2,500 wamepoteza maisha au hawajulikani waliko wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania mwaka huu - idadi hiyo ikiwa juu zaidi ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2022.
Mkutano huo wa Malta unajiri pia wakati mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanakaribia kuafikiana juu ya pendekezo la sheria mpya ya jinsi Umoja huo utakavyoshughulikia suala la waomba hifadhi na wahamiaji, huku makubaliano juu ya hilo yakitarajiwa kufikiwa katika siku zijazo.
Kumekuwepo na msukumo mpya wa kufikia makubaliano juu ya pendekezo la sheria hizo mpya hasa kufuatia ongezeko la wahamiaji katika kisiwa kidogo cha Italia cha Lampedusa mapema mwezi huu.
Serikali ya Meloni inayoegemea siasa za mrengo mkali wa kulia, iliyochaguliwa kutokana na sera yake ya kupinga wahamiaji, imevutana na Ujerumani na Ufaransa huku Meloni akishinikiza nchi nyengine za Umoja wa Ulaya kugawanya mzigo wa kuwahudumia wahamiaji.
Hadi kufikia sasa, idadi ya wahamiaji waliowasili katika kisiwa cha Lampedusa imepindukia 133,000.