1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G7 kuilenga sekta ya mafuta ya Urusi

27 Juni 2022

Viongozi wa kundi la mataifa yaliyostawi kiviwanda na kidemokrasia la G7 wanaokutana nchini Ujerumani wanatarajiwa kutangaza hatua mpya za kuongeza mbinyo dhidi ya Urusi kutokana na dhima yake kwenye mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4DIb1
Deutschland I G7-Gipfel auf Schloss Elmau in Garmisch-Partenkirchen
Viongozi wa kundi la G7 na wakuu wa taasisi za Umoja wa Ulaya wakishiriki mkutano kusini mwa Ujerumani.Picha: Ludovic Marin/AFP

Viongozi hao wanaokutana tangu jana kwa mkutano wa kilele katika kitongoji cha Schloss Elmau kusini mwa Ujerumani wataitumia siku ya pili ya mkutano wao kujadili na kufikia makubaliano ya kuchukua hatua ziada dhidi ya Urusi wanayoitwika dhima kwa vita vya nchini Ukraine.

Maafisa wanaohudhuria mkutano huo wamesema viongozi wa kundi la G7 watailenga zaidi sekta ya mafuta ya Urusi kwa kukubaliana kuweka ukomo wa bei kwa bidhaa hiyo ambayo mataifa ya magharibi yanaamini yanaifaidisha sana Moscow.

Afisa mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema viongozi wa G7 wanakaribia kufikia makubaliano yatakayowaelekeza mawaziri wa sekta husika wa mataifa ya kundi hilo kutengezea mfumo utaoweka kikomo cha bei ya mafuta ya Urusi kwenye soko la dunia.

Lengo ni kuinyima Urusi mapato makubwa inayoyapata kutoka kwenye sekta hiyo kwa kupunguza bei ya mafuta.

Kadhalika viongozi wa G7 watajadiliana jinsi ya kuidhibiti Urusi kutumia teknolojia mamboleo kutoka mataifa ya magharibi katika sekta yake ya ulinzi.

Marekani tayari imetangaza njia za kufanya hivyo na kwa kuanza imesema itaweka vikwazo vitavyozuia uwezo wa Urusi kupata tena silaha inazitumia kuishambulia Ukraine.

Kundi la G7 lazungumzia mshikamano usioyumba kuhusu Ukraine

G7 Gipfel Schalte mir Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky akizungumza na viongozi wa kundi la G7 Picha: Tobias Schwarz/AFP

Hapo jana rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky alijiunga kwenye mkutano huo kwa njia ya video na kuwatolea mwito viongozi wa G7 kutoitupa mkono nchi yake.

Aliomba kupatiwa msaada ziada wa kifedha na silaha na kuiwezesha nchi yake kusafirisha shehena ya nafaka ambayo imekwama kutokana na vita inayoendelea.

Mwenyeji wa mkutano huo kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema baada ya ufunguzi wa mkutano huo kuwa suala la Ukraine ni kipaumbele kwa kundi la G7

"Tunajadili masuala yote yaliyo kwenye ajenda, hususani kuendeleza mshikamano wa kuisaidia Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi na tunaelewa kuwamba sera za mataifa yetu zinafanana sana. Nadhani huu ni ujumbe mzuri, kwamba tunachukua maamuzi magumu." amesema Scholz.

Mkutano wa G7 kukamilika siku ya tamko la pamoja 

G7 Gipfel Elmau
Picha: Christinan Bruna/Getty Images

Katika hatua nyingine ya kuiadhibu Urusi viongozi wa kundi la G7 wanapanga kuzielekeza fedha zilizopatikana hivi karibuni kupitia nyongeza ya ushuru wa biashara kwa bidhaa za Urusi zinazoingizwa kwenye mataifa ya magharibi kwenda kuisadia Ukraine. 

Rais wa Marekani Joe Biden amesema fedha hizo zitatuma kuisadia Ukraine kufidia gharama za uharibifu uliotokana na vita.

Ingawa suala la Ukraine ndiyo limegubika majadiliano ya G7,viongozi wa kundi hilo wamejadili pia masuala ya biashara duniani, msaada zaidi kwa bara la Afrika, usalama wa chakula na mfumuko wa bei.

Mkutano huo unaowakutanisha viongozi wa mataifa ya Ujerumani, Uingereza, Marekani, Ufaransa, Japan, Canada na Italia utamalizika kesho kwa kutolewa tamko la pamoja juu ya masuala chungunzima yatakayoafikiwa.